HOTUBA YA KAMISHNA WA MAADILI BARAZA LA WAFANYAKAZI MACHI 2025
HOTUBA YA KAMISHNA WA MAADILI, JAJI (Stahiki) SIVANGILWA S. MWANGESI KATIKA UFUNGUZI WA MKUTANO WA BARAZA LA WAFANYAKAZI WA SEKRETARIETI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA TAREHE12/03/2025 – UKUMBI WA MIKUTANO JENGO LA MAADILI- DODOMA
NDUGU,
MAKATIBU,
WAKUU WA IDARA NA VITENGO,
MAKATIBU WASAIDIZI,
VIONGOZI WA TUGHE,
WAJUMBE WA BARAZA LA WAFANYAKAZI,
WAGENI WAALIKWA,
MABIBI NA MABWANA.
Nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania!
Awali ya yote, ninamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia kuwepo leo hii tukiwa na Afya njema.
Niwashukuru Watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kutimiza wajibu wenu ipasavyo kwa uadilifu na weledi.
Natoa pongezi kwa waandaaji wa Mkutano huu, kwa maandalizi mazuri na kufanikisha kufanyika kwake.
Ninatambua huu ni mkutano wa pili wa Baraza la Wafanyakazi kwa mwaka wa fedha 2024/2025. Nawakaribisha wote katika Jengo letu ambapo ni Ofisi za Makao Makuu na Kanda ya Kati kwa wale ambao wanafika kwa mara ya kwanza.
Ndugu Wajumbe;
Mabaraza ya Wafanyakazi yameundwa kisheria kwa madhumuni ya kuishauri Serikali katika ngazi ya Taasisi ili kusimamia rasilimali na utekelezaji wa majukumu ya kila Taasisi ya Umma. Ninawaomba wajumbe wote mtumie fursa hii ya kuwawakilisha wenzenu vizuri ili Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma iweze kufikia malengo iliyojiwekea katika utekelezaji wa majukumu yake na kukidhi matarajio ya wananchi kwa ujumla.
Kukusanyika kwenu hapa iwe ni sehemu muhimu katika kuboresha mazingira ya kazi na pia kuongeza ufanisi na tija katika Taasisi yetu. Uzoefu umeonesha kuwa Mabaraza ya Wafanyakazi yanapotumika vyema, hali ya maelewano na utulivu mahali pa kazi huongezeka na hivyo kuongezeka kwa tija.
Ndugu Wajumbe;
Katika mkutano huu tutapata nafasi ya kupata uelewa kuhusu utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2024/2025 na Mwelekeo wa bajeti ya mwaka 2025/2026. Pia tutapokea taarifa ya Mfuko wa Kusaidiana na tutapatiwa elimu kuhusu mfuko wa amana wa UTT AMIS. Nawasihi kutumia vizuri muda huu kwa ajili ya kuchangia mawazo ambayo yataongeza tija kwa Taasisi yetu
Ndugu Wajumbe;
Pamoja na kuwa tumekutana maalumu kwa ajili ya kupokea na kujadili utekelezaji wa bajeti ya Taasisi 2024/2025 na mwelekeo wa Bajeti 2025/2026 lakini ni fursa pia ya kukumbushana machache kuhusu namna bora ya utekelezaji wa majukumu yetu kwa mtumishi mmoja mmoja na Taasisi kwa ujumla.
Ninafahamu kuna baadhi yetu wana changamoto za kiuadilifu katika utendaji wao, lakini kwakuwa Taasisi yetu tunayoitumikia ni ya kimaadili basi hatuna budi kukumbushana kwa lengo la kujipa muda kujitathmini na kujirekebisha kwenye suala la uaminifu, nidhamu, kupendana pamoja na utii kwa mamlaka na viongozi waliopo juu yetu kwa kuwa hayo yote yana athari chanya katika utekelezaji wa majukumu yetu na taswira ya Taasisi yetu kwa ujumla.
Aidha, nasisitiza kwenu wajumbe mkawe mabalozi kwa watumishi wengine kwenye suala la ujazaji wa majukumu katika mfumo wa e-utendaji ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Serikali na pia Waraka wa Ndani Na. 1 wa Mwaka 2025 ambao umetenga siku maaalum ya Alhamisi ya kila wiki kwa ajili ya kuingiza taarifa za utendaji kazi katika mfumo.
Ifahamike kuwa jukumu kubwa la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ni kusimamia Maadili ya Viongozi wa Umma, hivyo ni muhimu kwa watumishi wa Taasisi yetu kuwa mfano wa kuigwa katika uzingatiaji wa maadili. Hii ni katika kutekeleza Kanuni ya pili ya Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma za mwaka 2023 “UTII KWA SERIKALI” ambapo mtumishi anapaswa kuzingatia na kutekeleza Sera, Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayoongoza utendaji kazi ikiwa ni kupokea na kutekeleza maagizo halali yanayotolewa na Viongozi wa Serikali.
Ndugu Wajumbe,
Kwa kuwa tumekubali kuwa watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, niwakumbushe kwa mara nyingine kuwa tunawajibika kuzingatia nidhamu, uaminifu, uwazi na kupendana; atakayeenda tofauti na hayo atakuwa si miongoni mwetu na hatutasita kuchukua hatua stahiki.
Pamoja na changamoto nyingi tunazokabiliana nazo katika kazi yetu ya kusimamia uadilifu, ninawaomba tusikubali kuyumba au kuyumbishwa na hatimaye kutolewa kwenye mstari, tuendelee kufuata misingi ya weledi na maadili katika utendaji kazi kwa kuepukana na rushwa na kushinda vishawishi vya rushwa na tamaa nyinginezo.
Ndugu Wajumbe;
Binafsi nawapongeza kwa ushirikiano ambao mmenionesha. Ninaomba ushirikiano huo uendelee. Kwa upande wangu mlango uko wazi pale kwenye changamoto yoyote msisite kuniona ili tuijadili kwa pamoja na kuipatia ufumbuzi kwa ajili ya maendeleo ya Sekretarieti katika mchango wake wa KUDUMISHA UTAWALA BORA.
Aidha, kama mnavyonipa ushirikiano naomba ushirikiano huo uwe miongoni mwenu pia ili Taasisi ifike mbali.
Ndugu wajumbe,
Mwisho ninawashukuru kwa kuhudhuria na kila mmoja aendelee kufanya kazi kwa uadilifu, ubunifu na uzalendo wa hali ya juu kuhakikisha kuwa Taasisi yetu inafikia malengo yake. Ninawatakia majadiliano mema na yenye kujenga.
Baada ya kusema hayo, sasa natamka rasmi kuwa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, UMEFUNGULIWA RASMI.
AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA