KIONGOZI MMOJA AFIKISHWA MBELE YA BARAZA LA MAADILI
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imemfikisha mbele ya Baraza la Maadili Mkuu wa Idara ya Mipango wa Halmashauri ya wilaya Mbogwe mkoani Geita kwa kukiuka Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Bw. Alex Manyama Mang’ara aliyekabiliwa na mashtaka manne tofauti alifikishwa mbele ya Baraza la Maadili tarehe 14 Januari 2026 katika ukumbi wa ofisi za Sekretarieti ya Maadili jijini Dodoma kujibu tuhuma zinazomkabili.
Wakili Mkuu wa Serikali Bw. Hassan Mayunga ameliambia Baraza kuwa Bw. Alex Manyama bila sababu za msingi ameshindwa kutimiza matakwa ya kifungu cha 6(1)(a) na 6(1)(c) vya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma hivyo, kukiuka maadili ya uongozi wa umma kwa mujibu wa kifungu cha 6(2) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
“Wakati akikaimu nafasi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbongwe na akitekeleza majukumu yake alimuhamisha kituo cha kazi mtumishi wa Halmashauri hiyo Bi. Asifiwe Chipata na kumshusha cheo bila kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.”
Wakili Mayunga aliongeza kuwa, “Kitendo hicho ni kinyume na kifungu cha 6(1) (c) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kinachosomeka pamoja na kanuni ya 3(2)(a) ya kanuni za udhibiti wa Mgongano wa Maslahi.”
Aidha, Wakili Mayunga alilieleza Baraza la Maadili kuwa, Mlalamikiwa pia alimhamisha kituo cha kazi mtumishi mwingine wa Halmashauri hiyo Bi. Mercy Kabaka na kumshusha cheo bila kuzingatia sheria, kanuni na taratibu kinyume na kifungu cha 6(1)(c) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kinachosomeka pamoja na Kanuni ya 3(2)(a) ya Kanuni za Udhibiti wa Mgongano wa Maslahi.
Shtaka jingine linalomkabili Bw. Alex Mangara ni kumpanisha cheo Bw. Mohamed Manawa mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Bi. Mercy Kabaka aliyemhamisha na kumshusha cheo.
“Mhe. Mwenyekiti wa Baraza la Maadili, kitendo hicho ni kinyume na kifungu cha 6(1)(c) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kikisomeka pamoja na Kanuni ya 3(2)(b) ya Kanuni za Udhibiti wa Mgongano wa Maslahi,” alisema.
Kosa la nne pia linalomkabili Bwa. Alex ni kummpandisha cheo Bw. Edmund Kowi mtumishi wa Halmashauri ya Mbogwe kuziba nafasi ilioachwa wazi na Bi. Asifiwe Chipata aliyemuhamisha na kumshusha cheo.
Kwa mujibu wa maelezo ya shtaka hilo, kitendo hicho ni kinyume cha kifungu cha 6(1)(c) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kikisomeka pamoja na Kanuni ya 3(2)(b) ya Kanuni za Udhibiti wa Mgongano wa Maslahi.
Baada ya kusomewa mashtaka, Mhe. Rose Teemba, Mwenyekiti wa Baraza la Maadili alimuuliza mlalamikiwa kama amesikia mashtaka dhidi yake na kama anakiri kutenda kosa, Mlalamikiwa alisema, “ni kweli nimesikia mashtaka dhidi yangu na ninakiri kutenda hayo makosa.”
Bw. Alex alisema, “kwa kuwa maelezo yote yaliyosemwa na vifungu vya sheria vilivyotamkwa sina neno zaidi ya kuomba kusamehewa. Nilifanya hivyo kwa kukosa umakini.”
Aidha, Mhe. Teemba alisema, kwa kuwa maelezo yametolewa na umekiri kwa kinywa chako, Baraza litafanyia kazi shauri hili. Unaweza kwenda.”
Baraza la Maadili linaongozwa na Mhe. Jaji (Mst.) Rose Teemba, akisaidiana na Wajumbe wa Baraza hilo Bi. Suzan Mlawi na Bw. John Samwel Mgetta.
Upande wa mashtaka uliwakilishwa na Wakili Mkuu wa Serikali Bi. Emma Gelani, Bw. Hassan Mayunga, Lydia Mwakibete na Catherine Tibasana.
