Historia
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ni Idara ya Serikali inayojitegemea chini ya Ofisi ya Rais iliyopewa mamlaka ya kuchunguza tabia na mwenendo wa kiongozi wa umma yeyote kwa madhumuni ya kuhakikisha kuwa masharti ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma yanazingatiwa ipasavyo. Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ilianzishwa chini ya Ibara ya 132 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Sekretarieti ya Maadili imepewa mamlaka ya kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya 1995 sura 398. Sheria hii ilianza kutumika tarehe 01 Julai 1995 na inatumika Tanzania Bara pamoja na Zanzibar kwa viongozi wenye madaraka katika Serikali ya Muungano.
Sekretarieti ya Maadili inaongozwa na Kamishna wa Maadili ambaye huteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, Rais huwezesha kupatikana kwa watumishi wengine wa Sekretarieti ya Maadili ambao huwajibika kula kiapo cha kutunza siri zinazohusiana na majukumu ya taasisi.
Taasisi ina ofisi ya Makao Makuu iliyopo Dodoma pamoja na ofisi nane za Kanda kama ifuatavyo;
- Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yenye mikoa ya Mbeya, Iringa, Katavi, Songwe, Njombe na Rukwa.
- Kanda ya Kusini yenye mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma.
- Kanda ya Kati yenye mikoa ya Dodoma na Singida.
- Kanda ya Kaskazini yenye mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara.
- Kanda ya Magharibi yenye mikoa ya Tabora, Kigoma, Simiyu na Shinyanga.
- Kanda ya Ziwa yenye mikoa ya Mwanza, Mara, Geita na Kagera.
- Kanda ya Mashariki yenye mikoa ya Tanga na Morogoro.
- Kanda Maalum yenye mikoa ya Dar Es Salaam na Pwani pamoja na Unguja na Pemba.