JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA RAIS – SEKRETARIETI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA

Maswali

1. Kuhusu utoaji wa Tamko la Rasilimali na Madeni, kuna changamoto ya Wenza kusaidia kupatikana kwa Taarifa za Tamko. Je, Mwenza asipowezesha kutoa taarifa sahihi itakuwaje?

Jibu: Kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, jukumu ama wajibu wa kutoa tamko la rasilimali na madeni ni kwa kiongozi wa umma, ambaye anatakiwa kutoa tamko hilo juu ya rasilimali na madeni yake, ya mwenza/wenza wake, na watoto wake wenye umri chini ya miaka 18 ambao hawajaoa ama kuolewa. Mali zinazotakiwa kutolewa tamko ni pamoja na fedha taslimu, fedha zilizopo katika taasisi za kifedha kama vile benki, hisa, nyumba, mashamba, magari, viwanja, mitambo, na shughuli nyinginezo halali anazojishughuisha nazo. Endapo kiongozi atatumia majina ya mwenza, watoto au ndugu kuficha mali zake na akabainika kiongozi huyo atawajibishwa kwa mujibu wa sheria.

 

Ni jukumu la kiongozi husika kumwelimisha mwenza wake kuhusu matakwa ya sheria ya maadili ili kumpatia ushirikiano katika kutekeleza sheria hiyo, endapo mwenza huyo hataelewa, kiongozi anashauriwa kuwasiliana na Ofisi ya Kamishna wa Maadili ili kupata ushauri zaidi. Endapo kiongozi wa Umma atashindwa kutoa taarifa zinazomilikiwa na mwenza/wenza kwa sababu mwenza huyo ameficha taarifa hizo/ ama hajawezesha kupatikana kwa taarifa husika, hatua za kisheria zitachukuliwa kwa atakayekuwa amehusika kuzuia utekelezaji wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

 

2. Katika kipindi cha miezi sita ya kusubiria (Cooling off Period). Je, hairuhusiwi kiongozi kufanya shughuli nyingine yoyote?

 

Jibu: Kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Kanuni ya 3(2)(g) ya Kanuni za Udhibiti wa Mgongano wa Maslahi 2020, kiongozi wa umma anapokuwa amestaafu au ameacha utumishi wa umma, ndani ya kipindi cha miezi sita tangu ameacha utumishi huo, (cooling off period), hataruhusiwa kuajiriwa, kujitolea, ama kujishughulisha na ajira kwa namna nyingine yoyote katika kampuni, watu ama ofisi yoyote inayofanya kazi na ofisi ya umma ambayo kiongozi huyo alikuwa akifanyia kazi alipokuwa madarakani.

 

3. Kuhusu malipo ambayo kiongozi hajalipwa na mwajiri wake wa zamani, je ayatamke kama madeni ya namna gani?

Jibu: Sheria inamtaka kiongozi wa umma kutamka rasilimali, maslahi na madeni yake anayodai ama anayodaiwa. Kama kuna malipo ambayo kiongozi hajalipwa, na anamdai mwajiri wake wa zamani ama wa sasa, ama anamdai mtu mwingine yeyote, kiongozi ataelezea deni hilo limetokana na nini pamoja na kiasi cha deni/madeni husika anachodai kwa mwajiri huyo. Vivyo hivyo endapo kiongozi anadaiwa na mwajiri, ama mtu mwingine yeyote atatamka deni hilo na kiasi anachodaiwa.

 

4. Kuhusu Tamko la Rasilimali na Madeni kwa Viongozi wapya, siku thelathini zinaanzia kuhesabika siku ya kuteuliwa au baada ya kuapishwa?

 

Jibu: Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma inamtaka kiongozi wa umma kutoa Tamko la rasilimali, masilahi na madeni ndani ya kipindi cha siku thelathini tangu kuteuliwa kwake katika nafasi aliyopewa. Kwa kawaida uapisho wa kiongozi aliyeteuliwa, hufuata mara baada ya uteuzi kufanyika, na uapisho unapofanyika ni ishara ya kiongozi anayoitoa kwa umma ya kuikubali dhamana pamoja na kuwajibika kwa nafasi aliopewa.

 

5. Ushauri kuhusu Tamko la Rasilimali na Madeni, Wenza wajaze matamko yao wenyewe. Je, inaruhusiwa?

Jibu: Viongozi wa Umma wanaowajibika na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, wametajwa katika Kifungu cha 4(1) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Aidha Gazeti la Serikali Na. 857 la tarehe 24 Novemba, 2023 limeorodhesha viongozi wanaowajibika na sheria hiyo, kwa kutaja vyeo vyote ambavyo viongozi wenye vyeo hiyvo wanapaswa kuwajibika na sheria ya maadili ikiwepo kutakiwa kutoa tamko la rasilimali, maslahi na madeni. Kwa mujibu wa sheria hiyo, Wenza wa Viongozi wa umma ambao hawana dhamana ya uongozi katika utumishi wa umma, hawapaswi na hawaruhusiwi kutamka rasilimali, maslahi na madeni yao binafsi kwa vile wao siyo viongozi wa umma kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Sheria inamtaka Kiongozi wa Umma kutamka rasilimali, maslahi na madeni yake, mweza/wenza wake na watoto wake walio chini ya umri wa miaka 18 ambao hawajaoa ama kuolewa.

6. Ni nini sababu ya kutoa tamko miezi mitatu kabla ya kustaafu?

Jibu: Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma inamtaka kiongozi wa umma kutoa tamko la rasilimali, maslahi na madeni katika vipindi vitatu: Kipindi cha siku thelathini tangu alipoteuliwa au kuchaguliwa; Kila ifikapo tarehe 31 Desemba ya kila mwaka, na kwa kipindi cha siku tisini kabla ya kustaafu utumishi wake kwa umma. Lengo la matamko haya yote kwa pamoja ni kumwezesha kiongozi kutekeleza matakwa ya sheria ya maadili ya viongozi wa umma ambayo imeainisha aina za matamko hayo na namna ya kuyatoa. 

 

7. Je, kiongozi haruhusiwi kuwa na hisa?

Jibu: Sheria ya maadili ya Viongozi wa umma haijakataza viongozi kumiliki mali za aina yoyote zikiwemo hisa. Kiongozi wa umma anayo haki ya msingi na kikatiba kama raia mwingine yeyote kumiliki mali na kuhakikishiwa usalama wa mali zake. Kiongozi wa umma anachotakiwa kufanya ni kuwa muadilifu na kuhakikisha hisa ama mali nyingine zozote anazomiliki ni mali halali zinazotokana na kipato chake halali, na atoe tamko la hisa hizo, atamke idadi au kiasi cha hisa alizonazo, atamke kampuni yenye  hizo hisa, pamoja na gawio ama faida anazozipata kutokana na hisa hizo. Kiongozi asitumie madaraka ama wadhifa wake kujipatia mali ama kujilimbikizia mali kinyume cha sheria.

 

 

8. Ukikuta fedha zimewekwa kwenye Akaunti yako bila ufahamu ukazitumia, inakuwaje?

Jibu: Uendeshaji wa akaunti binafsi katika taasisi za fedha ni jukumu la mmiliki binafsi wa akaunti hiyo. Endapo fedha zimewekwa ama kutolewa katika akaunti husika bila mmililki wa akaunti kufahamu, mmiliki wa akaunti hiyo anapaswa kutoa taarifa mara moja kwa uongozi wa benki husika. Ni kosa kwa kiongozi ama mtu yeyote kutumia fedha zilizoingizwa kwenye akaunti yake ya benki bila kujua fedha hizo zilikotoka. Kwa kutoa taarifa mapema kwa uongozi wa benki, kutamwondolea kiongozi ama mmililki wa akaunti husika kuhusishwa na matukio yasiyofaa ya wizi wa fedha, kusafirisha fedha haramu ama kujihusisha na matukio ya utakatishaji fedha, ambapo hatua za kisheria zinaweza kuchukuliwa dhidi yake.  

 

 

9. Kama kuna taarifa ambazo bado kiongozi hajazipata ndani ya siku thelathini baada ya kupata wadhifa inakuwaje?

 

Jibu: Endapo kiongozi wa umma atakuwa hajapata baadhi ya taarifa za umiliki wa rasilimali, maslahi au madeni yake anayotakiwa kuyatolea tamko ndani ya siku thelathini kwa mujibu wa sheria, ama endapo atapata changamoto zozote katika kutekeleza matakwa ya sheria ya maadili ya viongozi wa umma katika kutoa tamko hilo, kiongozi huyo anaweza kuwasiliana na ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa ushauri.

 

10. Kuhusu kudhibiti Mgongano wa maslahi, Je, viongozi wakatae kupokea michango ya harusi au wajiondoe kushughulikia masuala ya wale waliowachangia?

 

Jibu: Mgongano wa Maslahi ni tatizo la kimaadili. Hata hivyo, Viongozi wa umma, hawapaswi kujitenga ama kuishi kwa kukwepa kushiriki matukio ya kijamii yanayotokea ndani ya jamii kwa kisingizio cha kukwepa ama kudhibiti mgongano wa maslahi. Viongozi wanashauriwa kushiriki matukio ya harusi, misiba, nk katika jamii wanamoishi kwa uadilifu, pamoja na kushirikiana na wanajamii wengine bila kujihusisha na mgongano wa kimaslahi, na endapo kiongozi atakuwa na mashaka juu ya ushiriki huo anaweza kuwasiliana na Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa ushauri juu ya suala hilo.

 

11. Waheshimiwa Majaji wanaruhusiwa kufanya biashara?

Jibu: Viongozi wa Umma hawapaswi kuishi kama kisiwa. Wanayo fursa kisheria kufanya  shughuli nyingine halali ili kuwaongezea kipato. Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma hajakataza kiongozi wa umma yeyote kujihusisha na biashara yoyote halali. Waheshimiwa Majaji na Viongozi wengine wanayo haki ya kufanya biashara. Wanaweza kufanya biashara, kununua hisa katika makampuni mbalimbali, kufanya shughuli za kilimo, ufugaji, nk. Ni jukumu la kiongozi husika kuona kwamba biashara ama shughuli nyingine anayoifanya ama anayotaka kuifanya ni halali na haitamzuia wala kuathiri kutekeleza ipasavyo majukumu na wajibu wake kwa umma.

 

 

12. Ni namna gani unaweza kushughulikia mgongano wa maslahi unaoweza kutokea kwa sababu ya biashara za familia au nafasi ya udhamini?

Jibu: Kiongozi wa Umma anatakiwa kujiepusha na Mgongano wa Maslahi katika maeneo yote ya biashara za familia ama nafasi za udhamini. Endapo familia inafanya biashara inayomsababishia kiongozi kuingia katika mgongano wa maslahi, kiongozi anapaswa kutamka maslahi hayo kwa mamlaka yake ya Nidhamu ama kwa Kamishna wa Maadili. Kwa mujibu wa Kanuni za Kudhibiti Mgongano wa Maslahi za mwaka 2020, masuala mbalimbali yameainishwa ya namna ya kiongozi kuepuka mgongano wa maslahi. Kanuni hizo zinampa kiongozi wa umma fursa ya kuwasiliana na Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ili kuomba ushauri kuhusu namna anavyoweza kufanya shughuli zake za biashara ama nyinginezo bila kujiingiza kwenye mgongano wa maslahi.

 

 

13. Ni hatua zipi zinachukuliwa kwa Viongozi wanaokiuka maadili?

Jibu: Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, inafanya kazi ya kusimamia maadili kwa viongozi wa umma. Viongozi wanaothibitika kukiuka maadili wanachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria. Kila mara Kamishna wa Maadili anapokuwa na malalamiko yaliyochunguzwa na kujiridhisha kwamba kiongozi amekiuka maadili, kiongozi huyo huitwa kwenye Baraza la Maadili ambalo ndicho chombo cha kisheria kinachosikiliza na kufanya maamuzi ya mashauri ya viongozi waliokiuka maadili, na taarifa ya Baraza hilo huwasilishwa kwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua zaidi za kinidhamu na kisheria kwa viongozi husika. Hatua zinazoweza kuchukuliwa dhidi ya Kiongozi wa umma aliyekiuka maadili, zimeainishwa katika Kifungu (8)(a-g) cha Sheria ya Maadili, ikijumuisha kuonywa, kushushwa cheo, kusimamishwa kazi, kufukuzwa kazi, kufikishwa mahakamani, nk.

14. Hivi ni kweli mwenye pesa ndio mwenye haki na mnyonge hawezipata huduma kwa haki? Msemo huo una ukweli kiasi gani?

Jibu: Wananchi wote wana haki sawa bila kujali hali yao ya kipato, katika kupata huduma za umma. Huduma nyingi za umma hutolewa bure, hata hivyo zipo baadhi ya huduma ambazo zinatakiwa kuchangiwa gharama kidogo kwa mujibu wa taratibu za taasisi husika zinazotoa huduma hizo. Ila kwa huduma ambazo ni za bure mwananchi hapaswi kudaiwa fedha, na endapo fedha zinadaiwa kwa huduma ambazo hotolewa bure, mwananchi watoe taarifa mara moja kwa mamlaka zinazohusika ikiwepo Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili inafanya kazi kwa kushirikiana na taasisi nyingine kama vile Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Jeshi la Polisi, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, nk., hivyo endapo mwananchi anaona kiongozi ama mtumishi wa umma anakiuka maadili kwa kuomba kupewa rushwa, ama kukataa kutoa huduma bila sababu za msingi, mwananchi atoe taarifa mara moja kwa Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi ama ofisi nyingine iliyotajwa hapo juu kwani Ofisi za Umma huwa zinafanya kazi kwa ushirikiano. Wananchi wanashauriwa kuwa tayari kutoa taarifa zinaweza kubaini watumishi na viongozi wanaokiuka maadili. Taarifa zinaweza kutufikia kwa mwananchi kufika moja kwa moja katika Ofisi zetu, kupiga simu, kuandika barua, ama kutuma taarifa kupitia link iliyopo kwenye tovuti ya Sekretarieti, www.maadili.go.tz

 

 

Online Help
Kuanzisha Enzi Mpya katika Udhibiti wa Sekta ya Michezo ya Kubahatisha nchini Tanzania
Ofisi ya maadili inafanya kazi na imewashughulikia viongozi wengi sana kupitia Baraza la Maadili ambalo pia liliendeshwa mwaka 2013 Novemba mkoani Tabora. Viongozi mbalimbali waliokuwa na tuhuma za ukiukaji wa maadili waliitwa kwenye Baraza na kuhojiwa na Baraza linatoa mapendekezo na kuyawasilisha mapendekezo hayo kwa Rais kwa ajili ya hatua zaidi za kinidhamu na kisheria kwa viongozi husika.

" >
Kifungu cha 11(1) cha Sheria ya Maadili kimeainisha wazi mali zinazotakiwa kutajwa kuwa ni fedha taslimu, fedha zilizopo katika taasisi za kifedha kama vile benki, hisa, nyumba, mashamba, magari, mitambo na mali nyinginezo. Kiongozi anatakiwa kutoa tamko la mali anazomiliki yeye mwenyewe, mke/mume na watoto walio chini ya umri wa miaka kumi na nane. Fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni zinatakiwa kujazwa kila mwaka na kiongozi hutumiwa fomu hizo na Ofisi ya Maadili na pia zinapatikana katika mtandao wa maadili yaani www.ethicssecretariat.go.tz. Sheria inamtaka kiongozi kutolea tamko madeni yake ili kuweza kujua kuwa kiongozi anamiliki mali zipi na pia kutambua kuwa amezipata vipi mali hizo ukilinganisha na kipato cha kiongozi husika. Kiongozi kuwa na mali nyingi si dhambi kwani hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetamka wazi kuwa kila raia ana haki ya kumiliki mali ila ofisi inataka kujiridhisha uhalali wa jinsi mali ilivyopatikana. Mapendekezo katika Katiba mpya yanasisitiza maadili kwa kutenganisha uongozi na biashara.

" >
Wananchi wengi wamejijengea dhana kuwa bila pesa huwezi kupata huduma ya kiserikali kitu ambacho si kweli kwani huduma nyingi za kiserikali zinatolewa bure kabisa ila cha msingi wananchi wanatakiwa kutoa taarifa katika vyombo husika pindi wanapotakiwa kulipia huduma ambazo zinatolewa bure. Jamii inatakiwa kubadilika na kuamini kuwa si lazima kutoa rushwa ndipo upate huduma. Wapo wananchi wengi ambao walileta malalamiko kama hayo na Ofisi ya Maadili iliyashughulikia, hivyo wananchi wasisite kutembelea Ofisi zetu kwa ajili ya kutoa taarifa kama hizo.

" >
Kutoa lugha chafu ni ukiukwaji wa maadili. Ndani ya Bunge kuna Kamati ya Maadili ambayo ipo kwa ajili ya kuwawajibisha wabunge wanaotoa lugha chafu. Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa upande wake ilifanya semina kwa wabunge ili kuwakumbusha mipaka ya utendaji kazi na maadili kwa ujumla, na tangu wakati huo matumizi ya lugha chafu bungeni yamepungua kwa kiasi kikubwa.

" >