JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA RAIS – SEKRETARIETI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA

HOTUBA YA KAMISHNA KWA WAHARIRI WA VYOMBO VYA HABARI
03 Jun, 2025 Pakua

HOTUBA YA JAJI (Stahiki) SIVANGILWA S. MWANGESI, KAMISHNA WA  MAADILI WAKATI WA UFUNGUZI WA MKUTANO NA WAHARIRI WA VYOMBO VYA HABARI NCHINI TAREHE 30 MEI, 2025 KATIKA UKUMBI WA PEACOCK HOTELI, DAR ES SALAAM:

 

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF),

Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri,

Wahariri kutoka vyombo mbalimbali

Watumishi wa Sekretarieti ya Maadili wenzangu,

Waandishi wa habari.

Awali ya yote nitumie nafasi hii kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu muweza wa yote kwa kutukutanisha hapa tukiwa na afya njema kwa ajili ya mkutano huu muhimu wa kuzungumza nanyi mambo muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu. Taifa hili limejengeka katika misingi ya uadilifu ndio maana tuko hapa kuenzi misingi hiyo kwa kuelimishana, kujadiliana na kuendeleza pale tulipoishia katika kikao chetu cha tarehe 24 Mei, 2024 kilichofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania hapa Dar es Salaam.

Pili nitoe shukrani zangu za dhati kwa uongozi wote wa Jukwaa la Wahariri (TEF) chini ya Mwenyekiti wenu Deodatus Balile na Kamati Tendaji. Niwapongeze Wahariri walioshiriki katika mkutano wenu uliofanyika mjini Songea, mkoani Ruvuma mwezi Aprili mwaka huu kwa kuendelea kuonesha imani kwa Mwenyekiti wa TEF. Imani hii ni deni kubwa kwako kwani tasnia ya wanahabari itapenda kukukumbuka kwa kuivusha hapa ilipo nakuifanya kuwa chombo muhimu kinachotegemewa kuchangia maendeleo ya nchi yetu hasa suala la uadilifu wa viongozi wa umma.

Kitendo chenu cha kuitikia mwaliko wetu na kuja kwa wingi kubadilishana mawazo na sisi, ni kielelezo sahihi kuwa TEF ni mdau mkubwa wa maendeleo ya Taifa letu hususan kukuza maadili ya viongozi wa umma kutokana na nguvu za kalamu zenu.

Ndugu wahariri

Juhudi zenu katika ukuzaji wa maadili ya Viongozi wa Umma nchini zinaonekana wazi kwa jinsi mnavyotumia kalamu zenu kuelimisha, kuhabarisha, kuburudisha na kukosoa jamii kuhusu dhana ya uadilifu na uwajibikaji kwa Viongozi wa Umma. Kazi zenu zinasaidia kutupa vyanzo vya taarifa za kufanyia kazi.

Niwapongeze pia kwa kazi yenu nzuri mnayoifanya, ni kazi inayohitaji weledi katika mambo mbali mbali hususan katika kukuza maadili kwa kuchapisha habari zenye ukweli zikiwemo za uadilifu wa viongozi wa umma, uwajibikaji na wakati mwingine kukosoa baadhi ya mienendo isiyofaa ya baadhi ya Viongozi wa Umma. Kazi hii mnaifanya kwa uwezo mkubwa na uzalendo wa hali ya juu, hongereni sana.

Na toa rai kwenu endeleeni kutoa habari zinazohusu miendendo ya Viongozi wa Umma.

Nafahamu kuwa vyombo vya habari vinaweza kutumia njia mbalimbali kufikisha ujumbe kwa wananchi kuhusu hali ya uadilifu na uwajibikaji kwa Viongozi wa Umma nchini. Baadhi ya njia hizi ni vikaragosi, picha jongefu, tahariri, makala, nk.

Habari hizi zinasaidia viongozi kuzingatia matakwa ya Ibara ya 132 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 pamoja na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995.

Zipo taarifa nyingi tunazozifanyia kazi ambazo bila jitihada zenu, tusingezijua. Vyombo vya habari vimekuwa mdau na msaada wetu mkubwa katika kukusanya taarifa muhimu na za ukweli zinazoipa nguvu jamii kujua hali ya uadilifu nchini.

 

Ndugu wahariri

Kama nilivyosema hapo awali kuwa lengo letu kubwa ni kuelimishana na kubadilishana mawazo kuhusu uadilifu wa Viongozi wa Umma nchini. Pia tuna lengo la kuendeleza ushirikiano mwema kati ya Taasisi yetu na vyombo vyenu vya habari, kupitia kwenu nyinyi wahariri wa vyombo vya habari ambao jukumu lenu kubwa ni kupokea taarifa kutoka vyanzo mbali mbali na kuzichakata kabla ya kuzitangaza.

Majukumu ya Taasisi yetu ni pamoja na

  1. Kupokea malalamiko ya ukiukwaji wa maadili.
  2. Kupokea matamko ya raslimali, maslahi na madeni.
  3. Kufanya uchunguzi.
  4. Kutoa elimu ya maadili.
  5. Kufanya uhakiki.
  6. Kufanya utafiti wa hali ya uadilifu nchini.
  7. Kutoa ushauri katika mambo ya uadilifu na
  8. Kubuni mikakati ya ukuzaji wa maadili nchini.

Tunafanya hivi kuwajengea weledi wa kutosha ili mnaposikia jambo muwe na ufahamu wa kutosha kabla ya kulitangaza.

Hatua hii itasaidia kuongeza weledi na ulinganifu utakaozingatia uhuru wa kujieleza kwa kuzingatia Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Kanuni zake na misingi ya taaluma yenu ya habari.

Niwaombe kwa umoja wenu, kutumia ubunifu wa kalamu zenu kuandika habari nyingi zinazoeleza umuhimu wa maadili kwa Viongozi wa Umma nchini. Tuwaondolee viongozi na wananchi hofu tunapotimiza wajibu wetu kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zilizopo. Tusaidiane kukuza Uadilifu wa viongozi wetu, kwani uadilifu wa viongozi ukiongezeka utasaidia kukuza maendeleo ya taifa na kuongeza imani ya wananchi kwa Serikali yao.

Ndugu wahariri

Ni matumaini yangu kuwa tokea tulipokutana mara ya mwisho mwaka jana, yapo mengi ambayo mmeyapata hivyo leo mtatupa mrejesho.

Katika Mkutano wa mwaka jana tulizungumza kuhusu Taasisi yetu  kutekeleza majukumu kwa kutumia mifumo ya TEknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambapo tuliahidi kuanza kutumia mifumo hiyo. Katika utekelezaji wa majukumu yetu hasa upokeaji wa matamko kutoka kwa Viongozi wa Umma, tumeanza kutumia TEHAMA ambapo kwa sasa tunapokea matamko ya Viongozi wa Umma kwa njia ya mtandao yaani (Online Declaration System-ODS) kama mtakavyoelezwa katika mada itakayotolewa hapo baadaye.

Mfumo huu umeanzishwa ili kutekeleza Sera ya Serikali Mtandao (e – Government) ambayo Serikali imeagiza Wizara, Idara na Taasisi zote za Umma kutumia mifumo ya TEHAMA katika kurahisisha mawasiliano na utendaji kazi Serikalini.

Matumizi ya ODS ni hatua kubwa katika safari yetu ya maboresho na ubunifu wa kidigitali wa kujenga mifumo ya kuwajali wadau wetu kwa kuwapunguzia adha ya kutumia gharama kubwa na muda mwingi kuwasilisha Tamko la Rasilimali na Madeni.

Kwa nafasi hii, tunapenda kuwashukuru Viongozi wote wa Umma nchini kwa kuendelea kutupa ushirikiano tunapotekeleza majukumu yetu. Aidha, tunatoa shukrani zetu za pekee kwa wamiliki wa vyombo vya habari, Wahariri na Waandishi wa Habari kwa ushirikiano wao uliosaidia kuitambulisha ODS kwa umma.

Ndugu Wahariri

Najua mnafahamu kuwa mwaka huu ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani. Baada ya uchaguzi, tutapata viongozi watakaoliongoza Taifa hili kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Niwaombe mzingatie weledi wa taaluma yenu kwa kutoa taarifa sahihi, zenye ulinganifu zitakazosaidia wananchi kuchagua viongozi waadilifu.

 

Ahsanteni kwa kunisikiliza.

 

Online Help
Kuanzisha Enzi Mpya katika Udhibiti wa Sekta ya Michezo ya Kubahatisha nchini Tanzania
Ofisi ya maadili inafanya kazi na imewashughulikia viongozi wengi sana kupitia Baraza la Maadili ambalo pia liliendeshwa mwaka 2013 Novemba mkoani Tabora. Viongozi mbalimbali waliokuwa na tuhuma za ukiukaji wa maadili waliitwa kwenye Baraza na kuhojiwa na Baraza linatoa mapendekezo na kuyawasilisha mapendekezo hayo kwa Rais kwa ajili ya hatua zaidi za kinidhamu na kisheria kwa viongozi husika.

" >
Kifungu cha 11(1) cha Sheria ya Maadili kimeainisha wazi mali zinazotakiwa kutajwa kuwa ni fedha taslimu, fedha zilizopo katika taasisi za kifedha kama vile benki, hisa, nyumba, mashamba, magari, mitambo na mali nyinginezo. Kiongozi anatakiwa kutoa tamko la mali anazomiliki yeye mwenyewe, mke/mume na watoto walio chini ya umri wa miaka kumi na nane. Fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni zinatakiwa kujazwa kila mwaka na kiongozi hutumiwa fomu hizo na Ofisi ya Maadili na pia zinapatikana katika mtandao wa maadili yaani www.ethicssecretariat.go.tz. Sheria inamtaka kiongozi kutolea tamko madeni yake ili kuweza kujua kuwa kiongozi anamiliki mali zipi na pia kutambua kuwa amezipata vipi mali hizo ukilinganisha na kipato cha kiongozi husika. Kiongozi kuwa na mali nyingi si dhambi kwani hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetamka wazi kuwa kila raia ana haki ya kumiliki mali ila ofisi inataka kujiridhisha uhalali wa jinsi mali ilivyopatikana. Mapendekezo katika Katiba mpya yanasisitiza maadili kwa kutenganisha uongozi na biashara.

" >
Wananchi wengi wamejijengea dhana kuwa bila pesa huwezi kupata huduma ya kiserikali kitu ambacho si kweli kwani huduma nyingi za kiserikali zinatolewa bure kabisa ila cha msingi wananchi wanatakiwa kutoa taarifa katika vyombo husika pindi wanapotakiwa kulipia huduma ambazo zinatolewa bure. Jamii inatakiwa kubadilika na kuamini kuwa si lazima kutoa rushwa ndipo upate huduma. Wapo wananchi wengi ambao walileta malalamiko kama hayo na Ofisi ya Maadili iliyashughulikia, hivyo wananchi wasisite kutembelea Ofisi zetu kwa ajili ya kutoa taarifa kama hizo.

" >
Kutoa lugha chafu ni ukiukwaji wa maadili. Ndani ya Bunge kuna Kamati ya Maadili ambayo ipo kwa ajili ya kuwawajibisha wabunge wanaotoa lugha chafu. Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa upande wake ilifanya semina kwa wabunge ili kuwakumbusha mipaka ya utendaji kazi na maadili kwa ujumla, na tangu wakati huo matumizi ya lugha chafu bungeni yamepungua kwa kiasi kikubwa.

" >