Viongozi Tanesco wafurahia mafunzo ya maadili na uadilifu
Viongozi kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambao ni Mameneja wa Wilaya wamepongeza na kushukuru kwa kupatiwa mafunzo kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Viongozi hao wameyasema hayo katika mafunzo ya maadili na uadilifu kwa Viongozi wa Umma yaliyofanyika tarehe 9 Mei, 2026 katika ukumbi wa mikutano wa hoteli ya Vizano jijini Dodoma.
Akifunga Mafunzo hayo Kaimu Mkurugenzi wa Tanesco Kanda ya Kati Mhandisi William Msome amesema kuwa uongozi bora haupimwi kwa mafanikio bali katika kufanya maamuzi sahihi kwa kuzingatia kanuni, sheria, haki pamoja na usawa.
“Kupitia mafunzo haya tutakua mabalozi wazuri wa maadili na uadilifu, na tukafanye kazi kwa kufuata miongozo iliyopo na maamuzi yetu yasimamie haki na usawa ili kuleta huduma bora bila ya upendeleo kwa wananchi,” alisema.
Mhandisi Msome ameongeza kuwa wataendelea kushirikiana na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kuratibu mafunzo ya mara kwa mara ili kuendelea kuwakumbusha Viongozi na Watumishi wa Shirika hilo suala zima la maadili na uadilifu katika utendaji wao.
Kwa upande wake Mratibu Msaidizi wa mafunzo hayo kutoka Tanesco Bi. Stella Limbumba amesema kuwa mafunzo hayo yamekwenda vizuri, na imani yake kuwa washiriki watayafanya kuwa nyenzo katika utendaji wao na yeye kama sehemu ya wasimamizi kuna kitu amejifunza kupitia mafunzo hayo.
“Sio mara ya kwanza kwa Viongozi wetu kupata semina ya maadili na uadilifu, tunafanya hivi mara kwa mara ili kuwakumbusha na kuwaweka salama wakati wa kutekeleza majukumu yao, na pia ni mazuri kwa Viongozi wapya kuwasaidia katika utendaji wao mara baada ya kupata uteuzi wa kuwa Viongozi wa Umma,” alisema Bi. Stella.
Nae Meneja Tanesco Wilaya ya Uyui iliyopo mkoani Tabora Mhandisi Hamidu Saidi Juma ametoa shukrani zake kwa waratibu wa mafunzo hayo na kuongeza kuwa maarifa waliyopata ni msingi katika utendaji wao na watayatumia katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora kwa maendeleo ya Taifa.
“Kwa kweli mafunzo ni mazuri, tunawashukuru wawezeshaji wetu kwa kutoa mada zenye kueleweka na pia darasa lilikua shirikishi na elimu tuliyopata itatusaidia katika utendaji wetu ambao lengo ni kutoa huduma bora kwa wananchi na kujenga imani kwa Serikali,” alisema Mhandisi Juma.
Mafunzo hayo yaliyodumu kwa siku mbili yaliambatana na mada mbali mbali zilizowasilishwa na wawezeshaji kutoka Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kati Dodoma, ambao ni Katibu Msaidizi Bi. Jasmin Awadhi na Bw. Alfred Mboya ambaye ni Afisa wa ofisi hiyo.
