JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA RAIS – SEKRETARIETI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA

Sekretarieti ya Maadili Kuendeleza Ushirikiano na Vyombo vya Habari
31 May, 2025
Sekretarieti ya Maadili Kuendeleza Ushirikiano na Vyombo vya Habari

Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji (Stahiki) Sivangilwa Mwangesi amesema Sekretarieti ya Maadili itaendeleza ushirikiano na vyombo vya Habari nchini na kuvitaka kuendelea kuandika habari zinazoeleza umuhimu wa Maadili kwa Viongozi wa Umma.

Jaji Mwangesi amesema hayo wakati akifungua mkutano wa Jukwaa la Wahariri nchini wenye lengo la kutoa elimu na kuendeleza ushirikiano na Chombo hicho katika   kueleza kazi, majukumu na mafanikio ya Sekretarieti ya Maadili.

Mkutano huo ulifanyika tarehe 30 Mei, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya PEACOCK jijini Dar-es-Salaam.

‘’Sekretarieti ya Maadili inatambua juhudi kubwa za vyombo vya Habari katika kukuza Maadili ya Viongozi wa Umma nchini kwa kutumia kalamu zenu katika kuelimisha, kuhabarisha, kuburudisha pamoja na kukosoa kuhusu dhana ya Uadilifu na uwajibikaji kwa viongozi wa umma,’’alisema Jaji Mwangesi.

“Ndugu zangu Wahariri ni wazi zipo taarifa nyingi tunazozifanyia kazi kuhusu Viongozi wa Umma, ambazo bila jitihada zenu tusingezijua hii inaonyesha kuwa vyombo vya habari ni mdau na msaada mkubwa katika kukusanya taarifa muhimu na za ukweli zinazipa nguvu jamii kujua hali ya uadilifu nchini”. Aliongeza Mwangesi.

Aidha, Mwangesi amewaomba Wahariri kuendeleza weledi na kutumia taaluma zao kwa kutoa taarifa sahihi na zenye ulinganifu ambazo zitawasaidia wananchi kuchagua Viongozi waadilifu katika kipindi hiki ambacho nchi inaelekea katika Uchaguzi Mkuu baadae mwaka huu.

Kwa upande wake Katibu Msaidizi Ukuzaji wa Maadili, Bw. Fabian Pokela ametumia fursa hiyo kutoa elimu ya majukumu na kazi zinazofanywa na Sekretarieti ya Maadili na kutoa wito kwa Wahariri kusaidia kutoa elimu ya Maadili kwa jamii.

Nao, Wahariri wamemuomba Kamishna wa Maadili kuendelea kutoa elimu kwa umma ili jamii iweze kufahamu majukumu na kazi zinazofanyika na Sekretarieti ya Maadili.

Akiongea kwa niaba ya Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Bw. Salim Salim ameishukuru Sekretarieti ya Maadili kwa kuwaongezea uelewa wajumbe wake kuhusu masuala mbalimbali ya Maadili kwa Viongozi wa Umma yatakayo wasaidia kutekeleza vizuri majukumu yao.

 

 

Online Help
Kuanzisha Enzi Mpya katika Udhibiti wa Sekta ya Michezo ya Kubahatisha nchini Tanzania
Ofisi ya maadili inafanya kazi na imewashughulikia viongozi wengi sana kupitia Baraza la Maadili ambalo pia liliendeshwa mwaka 2013 Novemba mkoani Tabora. Viongozi mbalimbali waliokuwa na tuhuma za ukiukaji wa maadili waliitwa kwenye Baraza na kuhojiwa na Baraza linatoa mapendekezo na kuyawasilisha mapendekezo hayo kwa Rais kwa ajili ya hatua zaidi za kinidhamu na kisheria kwa viongozi husika.

" >
Kifungu cha 11(1) cha Sheria ya Maadili kimeainisha wazi mali zinazotakiwa kutajwa kuwa ni fedha taslimu, fedha zilizopo katika taasisi za kifedha kama vile benki, hisa, nyumba, mashamba, magari, mitambo na mali nyinginezo. Kiongozi anatakiwa kutoa tamko la mali anazomiliki yeye mwenyewe, mke/mume na watoto walio chini ya umri wa miaka kumi na nane. Fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni zinatakiwa kujazwa kila mwaka na kiongozi hutumiwa fomu hizo na Ofisi ya Maadili na pia zinapatikana katika mtandao wa maadili yaani www.ethicssecretariat.go.tz. Sheria inamtaka kiongozi kutolea tamko madeni yake ili kuweza kujua kuwa kiongozi anamiliki mali zipi na pia kutambua kuwa amezipata vipi mali hizo ukilinganisha na kipato cha kiongozi husika. Kiongozi kuwa na mali nyingi si dhambi kwani hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetamka wazi kuwa kila raia ana haki ya kumiliki mali ila ofisi inataka kujiridhisha uhalali wa jinsi mali ilivyopatikana. Mapendekezo katika Katiba mpya yanasisitiza maadili kwa kutenganisha uongozi na biashara.

" >
Wananchi wengi wamejijengea dhana kuwa bila pesa huwezi kupata huduma ya kiserikali kitu ambacho si kweli kwani huduma nyingi za kiserikali zinatolewa bure kabisa ila cha msingi wananchi wanatakiwa kutoa taarifa katika vyombo husika pindi wanapotakiwa kulipia huduma ambazo zinatolewa bure. Jamii inatakiwa kubadilika na kuamini kuwa si lazima kutoa rushwa ndipo upate huduma. Wapo wananchi wengi ambao walileta malalamiko kama hayo na Ofisi ya Maadili iliyashughulikia, hivyo wananchi wasisite kutembelea Ofisi zetu kwa ajili ya kutoa taarifa kama hizo.

" >
Kutoa lugha chafu ni ukiukwaji wa maadili. Ndani ya Bunge kuna Kamati ya Maadili ambayo ipo kwa ajili ya kuwawajibisha wabunge wanaotoa lugha chafu. Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa upande wake ilifanya semina kwa wabunge ili kuwakumbusha mipaka ya utendaji kazi na maadili kwa ujumla, na tangu wakati huo matumizi ya lugha chafu bungeni yamepungua kwa kiasi kikubwa.

" >