Sekretarieti ya Maadili yafungua Klabu mpya 20 za maadili wilayani Kongwa

Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kati-Dodoma imeanzisha klabu mpya 20 za maadili kwa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma.
Akiongoza zoezi la kuanzisha klabu hizo kati ya tarehe 13 hadi 15 Mei, 2025 Katibu Msaidizi, Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya kati Bi. Jasmin Awadhi amesema kuwa wamefanikisha kuzindua klabu hizo kwa ushirikiano mkubwa na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Dkt. Omary Nkullo.
‘’Lengo letu ilikua kufungua klabu 20 za maadili kwa Kata nne za Wilaya ya Kongwa ambazo ni Kata ya Kongwa, Ugogoni, Sejeli pamoja na Hogoro na mpaka tunavyoongea hapa ni kuwa tumefanikiwa kutimiza lengo hilo kwa kufungua idadi hiyo ya klabu 20 tulizojiwekea katika malengo yetu,’’ alisema Bi. Jasmin.
Bi. Jasmin ameongeza kuwa licha ya kufungua klabu hizo mpya 20 pia wamefanikiwa kuitembelea na kuhuisha klabu moja ya zamani iliyopo katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) wilayani humo na kuongeza kuwa wanaushukuru uongozi wa Wilaya ya Kongwa kwa kuwa bega kwa bega katika kufanikisha zoezi hilo ambalo ni endelevu.
Kati ya shule hizo 20 zilifanikiwa kupata klabu za maadili, shule za msingi ni 16 na shule nne ni za sekondari ambapo zipo katika kata hizo nne zilizofikiwa katika zoezi hilo ambapo takribani kila uongozi wa shule zote hizo umelipokea zoezi hilo kwa mikono miwili na kulifurahia kwa namna tofauti.
Shule za msingi zilizofanya uzinduzi wa klabu hizo ni Ubalozi, Viganga, Mlanga,Ibwaga, Padre Corado, Mnyakongo, Nguji, Mautya, Machenje, Sejeli, Msunjilile, Banyibanyi, Mkutani, chilingo, Tumaini pamoja na shule ya msingi Job Ndugai.
Kwa upande wa shule za sekondari zilizopata klabu za maadili ni pamoja na Msunjilile, Banyibanyi, Mnyakongo na Ibwaga.
Akizungumza mara baada ya kufunguliwa kwa klabu ya Maadili shuleni kwake, Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Tumaini Bw. Mussa Samweli Joseph ameipongeza Sekretarieti ya Maadili na kuishukuru kwa kuichagua shule yao kuwa miongoni mwa shule zilipata klabu za maadili wilayani humo na kuahidi kutoa ushirikiano katika kuiendeleza klabu hiyo.
‘’Kwanza niwapongeze na kuwashukuru kwa hatua hii na pia niwaombe muendelee kuwa na sisi pamoja na klabu nyingine mnazozisimamia ,kwani kwa namna hii itasaidia kupata Viongozi waadilifu na pia Raia wema na wazuri kwa kizazi cha baadae,’’ alisema Bw. Mussa.