Sekretarieti ya Maadili yashiriki kikamilifu Wiki ya Utumishi wa Umma 2025

Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imeshiriki katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2025 yaliyofanyika katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
Maadhimisho hayo yaliyozinduliwa rasmi Juni 17, 2025 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene (Mb) yamefika tamati Juni 23, 2025 ambapo mgeni rasmi alikua Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb).
Maadhimisho ya mwaka huu, yaliambatana na maonyesho kadha wa kadha kutoka katika Wizara, Taasisi za Umma, Sekretarieti za Mikoa, Asasi za Kiraia na Sekta Binafsi.
Katika maadhimisho hayo, Sekretarieti ya Maadili ilitoa elimu ya Sheria ya Maadili, Mgongano wa Maslahi pamoja na ujazaji wa Tamko la Rasilimali na Madeni kwa njia ya mtandao yaani Online Declaration System (ODS) kwa Viongozi wa Umma na wananchi waliotembelea banda la ofisi hiyo.
Baadhi ya wageni waliotembelea banda la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma walifurahia huduma iliyotolewa na kupongeza jitihada za ofisi hiyo katika kusimamia maadili nchini ikiwemo matumizi ya Mfumo wa ODS unaotumiwa na viongozi kujaza Tamko la Rasilimali na Madeni.
Mmoja wa Viongozi wa Umma aliyetembelea banda la Sekretarieti ya Maadili ni Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Kihenzile (Mb) ambaye amepongeza jitihada za Sekretarieti ya Maadili kuanzisha mfumo wa ODS ambao kwa mtazamo wake umeleta mabadiliko ya ujazaji wa Tamko la Rasilimali na Madeni kwa Viongozi wa Umma.
“Mnafanya kazi nzuri sana. Licha ya changamoto za kimtandao lakini nilifanikiwa kujaza tamko langu mapema na kwa wakati na kuliwakilisha kwa Kamishna wa Maadili. Rai yangu kwenu ni kuufanyia mfumo maboresho madogo madogo yanayoweza kuathiri ufanisi wake,’’ alisema Mhe. Kihenzile.
Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Dkt. Tausi Kida ameunga mkono matumizi ya Mfumo wa ODS na kushauri Sekretarieti kuandaa mafunzo maalum kwa wenza wa Viongozi ili nao wapate uelewa wa masuala ya ujazaji wa Tamko ili iwe rahisi nao kushiriki.
“Wenza wengi wa Viongozi hawafahamu vizuri jambo hili, hivyo naomba wakati wa kutoa mafunzo kwa Viongozi basi wenza wao wawepo ili waweze kupata uelewa wa namna suala hilo lilivyo na umuhimu kwa Kiongozi,’’ alisema.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deus Clement Sangu (Mb) ameipongeza Sekretarieti ya Maadili kwa kazi kubwa wanayofanya ya kusimamia maadili kwa Viongozi wa Umma nchini.
“Mnafanya kazi kubwa katika kuhakikisha Viongozi wa Umma wanazingatia maadili wanapotekeleza majukumu yao, nawapongeza katika hili na pia ninawaomba muendelee na kasi hii katika kuhakikisha tunakua na Viongozi waadilifu nchini,’’ alisema Mhe. Sangu.
Kuhusu Mfumo wa ODS, Naibu Waziri huyo amesema umeleta wepesi kwa vingozi na ameitaka Sekretarieti ya Maadili kuufanyia maboresho zaidi ili Viongozi waweze kujaza taarifa zao bila changamoto na kwa wakati.
“ODS inafanya vyema tofauti na mwanzo ambapo Viongozi walijaza kwenye makaratasi, kwa njia hii ya mtandao ni rahisi kuwasilisha Tamko kwa wakati, nakumbuka mwaka jana mfumo ulileta changamoto mwishoni na siku za kuwasilisha Tamko zikaongezwa, hivyo naomba mzifanyie kazi changomoto hizo kwa kuboresha baadhi ya maeneo ili mfumo uwe imara zaidi,’’ alisisitiza Mhe. Sangu.