Weledi, maarifa na jitihada vyatajwa katika kufanikisha malengo ya Taasisi na Taifa
Watumishi wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma wametakiwa kufanya kazi kwa weledi, maarifa na jitihada katika kufikia malengo ya Taasisi na Taifa kwa ujumla.
Rai hiyo imetolewa na Kamishna wa Maadili nchini Jaji (Stahiki) Sivangilwa Mwangesi wakati akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi hiyo makao makuu jijini Dodoma tarehe 18 Machi, 2026.
“Kila mtumishi kwa nafasi yake atekeleze majukumu yake kwa weledi, maarifa, jitihada na mapenzi, huku akitambua kuwa anategemewa kwa nafasi aliyonayo na kwamba yeye ni kipande au kiungo katika mkufu kwenye suala la kuleta maendeleo ya Taasisi na Taifa kwa ujumla,” alisema Mhe. Mwangesi.
Aidha Jaji Mwangesi ametumia nafasi hiyo kuwakumbusha watumishi wa ofisi hiyo kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kwa kushirikiana huku wakizingatia utunzaji siri za Serikali wanazozipata wakati wakitekeleza majukumu yao.
“Katika kufanikisha malengo ya Taasisi yetu na Taifa, suala la ushirikiano baina yetu halina mbadala hivyo ninaomba ushiriki wa kila mmoja katika kufanikisha malengo ya Taasisi na kujitaidi katika kutunza siri za Serikali,” alisisitiza Mhe. Mwangesi.
Mhe. Mwangesi ameongeza kuwa Katika kuendelea kutekeleza majukumu hayo ni vyema kila mtumishi wa ofisi hiyo kutambua kuwa wamepewa dhamana ya kuiwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake na kukumbuka kuwa Taasisi hiyo ndiyo taswira ya Taifa linapokuja suala la uadilifu.
“Ninaomba sote tufahamu kuwa katika utekelezaji wa majukumu yetu tunapokea maelekezo kutoka maeneo tofauti ambayo tunapaswa kuyatekeleza kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu na weledi na kwa kuwa tumeajiriwa ili tufanye kazi hivyo tuache uzembe, uvivu na mazoea na tuepuke kuwa chanzo au sababu ya kuikwamisha Serikali katika utendaji wake,” aliongeza Mhe. Mwangesi.
