Waziri Simbachawene azindua Makubaliano ya ushirikiano kati ya Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Chuo cha Uhasibu Arusha.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene (Mb) amezindua Mkataba wa Makubaliano ya ushirikiano katika nyanja mbalimbali kati ya Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA).
Uzinduzi huo umefanyia tarehe 6 Machi, 2025 katika ukumbi wa PSSSF jijini Dodoma.
Wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Simbachawene alisema kuwa makubaliano hayo yanaenda kuleta mwamko mpya kwa watu mbalimbali wa kuelewa suala la maadili na utawala bora kabla ya kushika nyadhida za uongozi wa umma.
“Nimeelezwa kuwa mmeingia makubaliano ya kutoa mafunzo kwa viongozi na watumishi wa umma katika nyanja mbalimbali, nitoe rai kuwa katika mafunzo yenu hakikisheni mnawaelimisha viongozi na watumishi matumizi sahihi ya mifumo iliyowekwa na Serikali kudhibiti mawasiliano ya ana kwa ana kati ya mtoa huduma na mpokea huduma. Uwepo wa mawasiliano ya ana kwa ana unachochea ukiukwaji wa maadili kwa kutoa ama kupokea rushwa na kusababisha kunyimwa haki kwa wanaostahili na kupatiwa wasiostahili,” alisema.
Aidha, Mhe Simbachawene alitoa raikwa IAA na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kutoa mafunzo ya matumizi sahihi ya rasilimali za nchi ili kupata mafanikio chanya katika Taifa.
“Sote ni mashahidi tunaona jinsi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan anavyopambana kuhakikisha kwamba nchi inakua na rasilimali za kutosha, lakini juhudi zake zinarudishwa nyuma na baadhi ya viongozi na watumishi wasiokua waadilifu wanaotumia rasilimali za nchi vibaya. Niwaombe mkawafundishe watumishi namna nzuri ya ugawaji na utumiaji wa rasilimali hizi kwa manufaa ya wote.”
Katika hatua nyingine, Mhe. Simbachawene alisema kuwa viongozi wote na watumishi wa umma wanapaswa kuwa mfano bora wa uwajibikaji, uwazi na utendaji haki kwani Taifa likiwa na Viongozi watenda haki tutajenga mfumo imara wa kuwahudumia wananchi kwa haki ili kujenga imani ya wananchi kwa serikali yao.
Katika maelezo yake ya utangulizi, Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji (Stahiki) Sivangilwa Mwangesi alieleza kuwa Mkataba wa Makubaliano kati ya Sekretarieti ya Maadili na Chuo cha Uhasibu Arusha, unalenga kuimarisha ushirikiano katika nyanja za utafiti wa maadili na utawala bora, utoaji wa ushauri wa kitaalam, machapisho kuhusu maadili na uongozi, pamoja na ujenzi wa mifumo madhubuti ya utawala bora.
Kwa mujibu wa Mhe. Mwangesi, mafunzo yatakayotolewa baada ya makubalianao hayo yatasaidia kuwaelimisha viongozi wa umma kuhusu umuhimu wa kuepuka mianya ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.
“Maarifa watakayopatiwa viongozi na watumishi wa umma, yatawasaidia kupata uwezo wa kutambua na kushughulikia changamoto za kimaadili zinazoathiri utendaji wao na jamii kwa ujumla,” alisema.
Katika hatua nyingine Mhe. Kamishna alisema kuwa pamoja na juhudi za serikali katika kuimarisha maadili, bado kuna changamoto zinazowakumba viongozi wa umma.
Amezitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na mgongano wa maslahi, matumizi mabaya ya madaraka, ushawishi wa kisiasa katika maamuzi ya kiutawala, na udhaifu wa mifumo ya usimamizi.
“Nitoe rai kwa kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa mifumo yetu ya uwajibikaji inaendelea kuimarishwa ili kuondoa changamoto hizi,” alisema.
Awali, Makamu Mkuu wa Chuo cha IAA Dkt. Grace Idinga alisema kuwa makubalianao yaliyozinduliwa leo, yanalenga maeneo matatu. Ameyataja maeneo hayo kuwa ni Kuimarisha uwezo wa viongozi na watumishi wa umma kuhusu maadili, ushauri, utafiti na Ushirikiano katika Utekelezaji wa Makubaliano.
“Ushirikiano wetu utaleta manufaa makubwa kwa taifa letu, ikiwemo kuimarisha utawala bora na maadili na kuboresha utoaji wa huduma kwa umma,”alisema.
Aidha, makubaliano hayo yaliyozinduliwa leo, yatachangia kujenga utumishi katika sekta ya umma na binafsi unaoongozwa na uadilifu, uwazi na uwajibikaji.