Wawezeshaji wa mafunzo ya maadili kwa Viongozi wa Umma watakiwa kuwa mabalozi wa mabadiliko ya maadili
Wawezeshaji wa mafunzo ya Maadili kwa Viongozi wa Umma wametakiwa kuwa mabalozi wa mabadiliko ya maadili katika utumishi wa umma.
Kauli hiyo imetolewa na Kamishna wa Maadili nchini Jaji (Stahiki) Sivangilwa Mwangesi wakati akifungua kikao kazi cha wawezeshaji wa mafunzo ya maadili kwa Viongozi wa Umma kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) jijini Arusha tarehe 6 Machi. 2026.
“Ushiriki wenu katika hili sio wa bahati mbaya, unaonyesha imani ambayo Taasisi hizi mbili zimeweka kwenu kutokana na utaalamu wenu pamoja na uwezo wenu wa kufundisha, kuhamasisha na kusimamia viwango vya juu vya maadili, hivyo ninyi sio wawezeshaji tu, bali pia ni mabalozi wa mabadiliko ya maadili katika utumishi wa umma,” alisema Mhe. Mwangesi.
Aidha Mhe. Mwangesi ameongeza kuwa wao kama wawezeshaji wa mafunzo ya maadili kwa Viongozi wa Umma kupitia wao Viongozi wa Umma wataweza kupata maarifa, misingi na miongozo ya maadili na hatimaye kujenga mfumo wa uongozi unaozingatia uwajibikaji, haki na uadilifu kwa manufaa ya Taifa.
“Kupitia ninyi Viongozi wa Umma wataweza kupata maarifa mbali mbali kuhusu maadili ,hivyo nawaomba kuongeza ubunifu katika mbinu mnazotumia katika kufundishia,” alisisitiza.
Awali akitoa neno la utangulizi Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) Prof. Eliamani Sedoyeka amesema kuwa lengo la kikao kazi hicho ni kupitia na kuboresha mpango kazi wa utoaji wa elimu ya maadili kwa Viongozi wa Umma ambao ulianza mwaka jana kwa ushirikiano kati ya Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
“Ni fursa nzuri kufanya kazi na Taasisi yenye jukumu nyeti la kusimamia maadili ya Viongozi wa Umma nchini, hivyo tupo hapa kupitia na kuangalia changamoto tulizopata katika awamu ya kwanza ambayo imemalizika vizuri licha ya changamoto za hapa na pale, na kisha kuboresha penye mapungufu,”alisema Prof. Sedoyeka.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo, Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu kutoka Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) Dkt. Grace Idinga amesema kuwa licha ya changomoto za hapa na pale walizopata katika awamu ya kwanza bado Viongozi walijitokeza kushiriki mafunzo hayo na wanatajia Viongozi wengi zaidi watajitokeza katika mafunzo ya awamu ya pili yanayotajiwa kuanza baadae mwezi huu.
“Viongozi 204 walijitokeza kushiriki katika awamu ya kwanza ya mafunzo haya, sawa na 24% ya malengo yetu,hivyo ni matarajio yetu awamu ya pili tutapata Viongozi wengi zaidi na pia tutafanyia kazi changamoto za awamu ya kwanza.” alisema Dkt. Grace.
