WAZIRI MKUU: MTANZANIA USIKUBALI KUTOA RUSHWA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amewataka watanzania wasikubali kutoa rushwa mahali popote huku akisisitiza kuwa wananchi ni wadau muhimu sana katika mapambano dhidi ya vita hiyo.
“Ninyi ni wadau wakubwa wa kukomesha rushwa, Nyie ni wadau wakubwa wa kukomesha vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu. Ili nchi yetu isiwe na vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa haki za binadamu, wananchi mnapaswa kufichua vitendo vya ukosefu wa maadili na uvunjifu wa haki za binadamu,” alisema.
“Mtanzania usikubali kutoa rushwa popote, hasa kwenye maeneo unayopaswa kupewa huduma hiyo. wewe ni mtanzania unalindwa na sheria za nchi za kupata huduma bure kama vile hospitali bila kutoa rushwa. Inatakiwa kila Mtanzania abebe jukumu hili kwa mikono miwili, alisimamie na alitekeleze,” alisisitiza.
Aidha Mhe. Waziri Mkuu alitoa wito huo wakati akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu yaliyofanyika katika viwanja vya Nyerere Square, jijini Dodoma tarehe 10 Disemba 2023.
Waziri Mkuu ambaye amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, alisema kuwa Mheshimiwa Rais amesisitiza umuhimu wa kila mmoja kuendelea kushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa na vitendo vingine vya ukiukwaji wa haki za binadamu. Maadhimisho ya mwaka huu yamebebwa na kaulimbiu isemayo:“Zingatia Maadili, Utu, Uhuru na Haki kwa Maendeleo Endelevu.”
Mhe.Waziri Mkuu aliendelea kusema kuwa kaulimbiu hiyo inachagiza masuala ya msingi yanayohusu maendeleo endelevu kutokana na ukweli kwamba kizazi huru chenye uadilifu, utu na kinazingatia haki ni msingi wa maendeleo ya Taifa lolote.
“Hivyo basi, hatuna budi wananchi wote kuunganisha nguvu katika ujenzi wa kizazi chenye misingi ya maadili. Kaulimbiu hii ni wito kwa sekta ya umma na sekta binafsi kutimiza wajibu wake kuhusu masuala ya maadili, utu, uhuru na haki. Kwa maneno mengine kaulimbiu hii imegusa taasisi zote na inasisitiza uwajibikaji wa kila mmoja wetu.”
Siku ya Maadili na Haki za Binadamu hapa nchini ilianza kuadhimishwa kwa pamoja mwaka 2016 ikiwa ni muunganiko wa siku mbili yaani siku ya Maadili na Haki za Binadamu.
Maadhimisho hayo huratibiwa na taasisi zinazosimamia utawala bora ikiwa ni pamoja na Ofisi ya Rais Ikulu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Wizara ya Katiba na Sheria, Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Tume ya Utumishi wa Umma, Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali pamoja na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.