Waziri Mhagama awataka Sekretarieti ya Maadili kujikita katika kutoa Elimu kwa Viongozi wa Umma.

Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imeaswa kujikita zaidi kutoa elimu kwa viongozi wa umma ili viongozi watii sheria bila shuruti.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama wakati alipofanya ziara ya kukagua mradi wa ujenzi wa Makao Makuu ya Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi Umma pamoja na Kanda ya Kati Dodoma tarehe 31 Machi, 2022 jijini Dodoma.
“Jukumu mlilopewa ni la kikatiba na sisi tumeona mnavyojitoa kuhakikisha maadili yanazingatiwa ipasavyo na Viongozi wa Umma.Unapoimarisha maadili ya Viongozi wa Umma unakuwa umeimarisha utawala bora”. Alisema Mhe. Mhagama.
Mhe. Mhagama aliendelea kufafanua kuwa angependa kuwekwe msisitizo katika kuwaondoa viongozi katika kukiuka maadili kwa kujikita zaidi katika kutoa elimu kuhusu maadili kwa viongozi ambao hawajui miiko ya viongozi.
“Azma ya Serikali ya Awamu ya sita inataka kila raia wa nchi hii atii sheria bila shuruti.Pia iwe ni wajibu wao kuzingatia sheria ili kufikia lengo la nchi kuwa na utawala bora”. Alisisitaza Mhe. Mhagama.
“Ingawa kuna malalamiko ya wananchi kuhusu ukiukwaji wa maadili unaofanywa na baadhi ya viongozi na nyie ni wajibu wenu kuchunguza malalamiko hayo ili kujua kama ni ya kweli”. Aliendelea kusema Mhe. Mhagama.
Kwa upande mwingine, Mhe. Mhagama aliwaasa watumishi wenyewe wa Sekretarieti ya Maadili kuwa na maadili ili kusaidia kusimamia maadili ya wengine na kuwataka kutenda haki kwa kuzingatia sheria wakati wanaposhughulikia malalamiko kwa sababu wanashughulikia maisha ya watu.
Pia, Mhe. Mhagama aliitaka Sekretarieti ya Maadili kutoa mrejesho kwa wananchi wanaolalamika kupitia mifumo iliyopo ya Serikali.
Aidha, Mhe. Mhagama aliendelea kubainisha kuwa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wameshaandaa mfumo unaoitwa ‘e-office’ na ni matumaini yake kuwa mifumo mengine katika taasisi nyingine za serikali zitajiunga na mfumo huo.
Kuhusu maendeleo ya Mradi wa ujenzi wa Makao Makuu ya Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambao kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Mkandarasi umefikia asilimia 50, Mhe. Mhagama alifurahishwa na hatua zilizofikiwa na ujenzi huo.
Hata hivyo Mhe. Mhagama alimtaka Mkandarasi wa Mradi huo ambaye ni Wakala wa Ujenzi Tanzania (TBA) kufanya kazi mchana na usiku ili kuharakisha ujenzi kwani Serikali inazo fedha za kutosha kukamilisha ujenzi wa jengo hilo na miradi mingine ya ujenzi wa majengo ya Serikali inayoendelea.
“Tumekubaliana hapa hakutakuwa na muda wa nyongeza kukamilisha mradi huu kwa sababu eneo gumu la kusimamsha ‘structure’ ya jengo tayari kilichobaki ni kuweka fremu, magrili na vitu vingine vidogovidogo na kuwataka kuzingatia ubora na thamani ya fedha za umma ambazo serikali imewekeza hapa” alimaliza kusema Mhe. Mhagama.