JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA RAIS – SEKRETARIETI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA

PO-ETHICS SECRETARIAT Logo
Waziri Kabudi; Viongozi wa Umma jiepusheni na mgongano wa maslahi
20 Feb, 2026
Waziri Kabudi; Viongozi wa Umma jiepusheni na mgongano wa maslahi

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu (Kazi Maalum) Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (Mb) amewaasa viongozi kuzingatia Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kuepuka mgongano wa maslah katika utendaji kazi wao.

Mhe. Kabudi amesema hayo tarehe 20.02.2026 wakati akifungua mafunzo ya maadili ya Viongozi wa Umma kwa Makatibu na Manaibu Katibu Wakuu wa Wizara yaliyofanyika katika ukumbi wa Sanaan jijini Dodoma.

“Viongozi wa Umma lazima watangulize maslah ya Umma badala ya maslah yao binafsi katika kipindi chote wanachokua madarakani hivyo, nawasihi kuzingatia  maadili na kushuhulikia vyema suala la mgongano wa maslah ili kudumisha imani ya umma kwa serikali na kuaminika kwa maamuzi yanayofanywa na Serikali,”alisema.

Katika hatua nyingine Mhe.Kabudi alieleza kuwa viongozi kushindwa kutenganisha uongozi na shughuli binafsi hasa za kibiashara ni kichocheo cha kutokea mgongano  kati maslah binafsi ya kiongozi wa umma na maslah ya umma jambo ambalo bado ni tatizo katika nchi yetu.

Katika hatua nyingine, Mhe. Kabudi alisema kuwa sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma haikutungwa ili kuwafanya Viongozi wawe maskini bali kudhibiti matumizi mabaya ya madaraka kwa viongozi wanaotaka kujinufaisha binafsi.

“Kiongozi kama walivyo raia wengine wa Tanzania ana haki ya kikatiba kumiliki mali na hifadhi ya mali yake kwa mujibu wa sheria. Kinachokatazwa ni Kiongozi wa Umma kutumia nafasi yake ya uongozi kujipatia mali isivyo halali,” amesema.

Mafunzo hayo yalikuwa na lengo la kukumbushana kuhusu umuhimu na wajibu wa viongozi wa umma kuzingatia maadili katika utekelezaji wa shughuli za Serikali.

“Ni muhimu kukumbushana na kubadilishana uzoefu kati ya wizara moja na nyingine kukabiliana na changamoto za kimaadili zinazojitokeza katika sekta zetu na kusababisha ubinafsi, tamaa, upendeleo na matummizi mabaya ya madaraka kwa baadhi ya watumishi wa umma ambao sio waadilifu,” amesisitiza.

Amewataka viongozi hao kujenga utumishi wa umma wenye sifa stahiki, uadilifu, uzalendo wa kitaifa, moyo wa kujituma, weledi, uwajibikaji na kufanya kazi kwa bidii kwa manufaa ya Taifa.

“Kwa nafasi za uongozi mlizonazo, umuhimu wenu katika kusimamia na kukuza maadili  katika sekta ya umma hauna mjadala wala mbadala.”

Katika hatua nyingine, Waziri Kabudi ameipongeza Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali ya kutumia mifumo ya TEHAMA kutoa huduma hasa Mfumo wa Ujazaji wa tamko la Rasilimali na Madeni kwa njia ya Mtandao (Online Declaration System - ODS).

Kwa mujibu wa Mhe. Kabudi ODS imewasaidia viongozi wengi wa umma kujaza tamko wakiwa mahali popote penye  huduma ya mtandao ndani au nje ya nchi.

“Kwa matumizi ya ODS, sidhani kama kuna kiongozi ambaye ana tashwishi kujaza tamko la Rasilimali na Madeni kwa mujibu wa sheria. Viongozi wa umma ambao hawajajaza au wamechelewa kujaza tamko watakuwa na sababu zao binafsi zaidi kuliko sababu za kimfumo,” amesema.

Awali, Kamishna wa Maadili Mhe.Jaji (Stahiki) Sivangilwa Mwangesi alieleza kuwa mafunzo hayo ni moja kati ya majukumu ya Sekretarieti ya Maadili kutoa elimu kwa viongozi wa umma kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

“Kupitia mafunzo haya, viongozi wanakumbushwa mambo wanayotakiwa kuzingatia wanapotimiza wajibu wao,” amesema.

Jumla ya mada mbili ziliwasilishwa katika mafunzo hayo ambazo ni  mada  kuhusu Changamoto za Kimaadili na nafasi ya watendaji wakuu wa Wizara kusimamia uadilifu katika sekta ya Umma na mada kuhusu udhibiti wa Mgongano wa Maslahi na uwajibikaji wa Viongozi wa umma kujenga utamaduni wa kimaadili Serikalini.

Online Help
Kuanzisha Enzi Mpya katika Udhibiti wa Sekta ya Michezo ya Kubahatisha nchini Tanzania
Ofisi ya maadili inafanya kazi na imewashughulikia viongozi wengi sana kupitia Baraza la Maadili ambalo pia liliendeshwa mwaka 2013 Novemba mkoani Tabora. Viongozi mbalimbali waliokuwa na tuhuma za ukiukaji wa maadili waliitwa kwenye Baraza na kuhojiwa na Baraza linatoa mapendekezo na kuyawasilisha mapendekezo hayo kwa Rais kwa ajili ya hatua zaidi za kinidhamu na kisheria kwa viongozi husika.

" >
Kifungu cha 11(1) cha Sheria ya Maadili kimeainisha wazi mali zinazotakiwa kutajwa kuwa ni fedha taslimu, fedha zilizopo katika taasisi za kifedha kama vile benki, hisa, nyumba, mashamba, magari, mitambo na mali nyinginezo. Kiongozi anatakiwa kutoa tamko la mali anazomiliki yeye mwenyewe, mke/mume na watoto walio chini ya umri wa miaka kumi na nane. Fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni zinatakiwa kujazwa kila mwaka na kiongozi hutumiwa fomu hizo na Ofisi ya Maadili na pia zinapatikana katika mtandao wa maadili yaani www.ethicssecretariat.go.tz. Sheria inamtaka kiongozi kutolea tamko madeni yake ili kuweza kujua kuwa kiongozi anamiliki mali zipi na pia kutambua kuwa amezipata vipi mali hizo ukilinganisha na kipato cha kiongozi husika. Kiongozi kuwa na mali nyingi si dhambi kwani hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetamka wazi kuwa kila raia ana haki ya kumiliki mali ila ofisi inataka kujiridhisha uhalali wa jinsi mali ilivyopatikana. Mapendekezo katika Katiba mpya yanasisitiza maadili kwa kutenganisha uongozi na biashara.

" >
Wananchi wengi wamejijengea dhana kuwa bila pesa huwezi kupata huduma ya kiserikali kitu ambacho si kweli kwani huduma nyingi za kiserikali zinatolewa bure kabisa ila cha msingi wananchi wanatakiwa kutoa taarifa katika vyombo husika pindi wanapotakiwa kulipia huduma ambazo zinatolewa bure. Jamii inatakiwa kubadilika na kuamini kuwa si lazima kutoa rushwa ndipo upate huduma. Wapo wananchi wengi ambao walileta malalamiko kama hayo na Ofisi ya Maadili iliyashughulikia, hivyo wananchi wasisite kutembelea Ofisi zetu kwa ajili ya kutoa taarifa kama hizo.

" >
Kutoa lugha chafu ni ukiukwaji wa maadili. Ndani ya Bunge kuna Kamati ya Maadili ambayo ipo kwa ajili ya kuwawajibisha wabunge wanaotoa lugha chafu. Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa upande wake ilifanya semina kwa wabunge ili kuwakumbusha mipaka ya utendaji kazi na maadili kwa ujumla, na tangu wakati huo matumizi ya lugha chafu bungeni yamepungua kwa kiasi kikubwa.

" >