WATUMISHI WAPYA WA SEKRETARIETI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA WAPEWA MAFUNZO KUHUSU UTUMISHI WA UMMA.
Watumishi wapya walioajiriwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na wale waliohamia kutoka katika Taasisi nyingine wametakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni, Sheria, taratibu na miongozo inayoongoza utumishi wa Umma kwa uadilifu na pia kwa kutumia ubunifu unaoendana na mabadiliko ya matumizi ya TEHAMA ili kufikia malengo ya Taasisi na Serikali kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa na Kamishna wa Maadili Mhe, Jaji (Mstahiki) Sivangilwa Mwangesi alipokuwa akifungua mafunzo kwa watumishi hao, yaliyofanyika tarehe 11 Novemba 2024 katika ukumbi wa ofisi za Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Makao makuu Dodoma.
Mhe, Mwangesi katika hotuba yake alifafanua kuwa, Serikali imeweka kanuni na miongozo ili watumishi waweze kuhudumia wananchi kwa utaratibu, uaminifu, usawa, haki na uwazi, hivyo, “mkiwa watumishi wa umma mna jukumu la kuzingatia kanuni hizo katika utendaji wenu wa kila siku.”
Aidha, Mhe. Mwangesi alibainisha kuwa, kutokana na unyeti wa taarifa zinazoshughulikiwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kila siku, suala la usalama wa taarifa ni jambo la msingi ambalo halina mbadala wala mzaha kulizingatia kwa uadilifu na umakini wa hali ya juu.
Mhe. Mwangesi katika hotuba yake aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia maarifa, elimu na maelekezo watakayopatiwa kutokana na umuhimu wake kuwa ndiyo mwongozo wa utendaji kazi katika utumishi wa umma.
Mafunzo hayo ya siku tatu yalitolewa na wakufunzi kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais Idara ya kumbukumbu na Nyaraka za Taifa