Watumishi wapya Sekretarieti ya Maadili watakiwa kufanya kazi kwa bidii na kwa Uadilifu mkubwa

Watumishi wapya walioajiriwa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma wametakiwa kuwa wabunifu, kufanya kazi kwa bidii, kuzingatia ushirikiano ili kutimiza malengo ya Taasisi na Serikali kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa na Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji (Stahiki) Sivangilwa Mwangesi alipokuwa akifungua mafunzo kwa watumishi hao yaliyofanyika tarehe 6 Oktoba, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa ofisi hiyo Makao Makuu Dodoma.
‘’Mkiwa kama watumishi wapya, mna jukumu muhimu la kutoa mawazo mapya hata kama ni madogo yanaweza kuwa na tija katika kuleta mafanikio ya pamoja na yote haya yatafanyika kama mtafanya kazi kwa bidii na ushirikiano katika kutekeleza majukumu yenu.’’ Alisema Mhe. Mwangesi.
Mhe. Jaji (Stahiki) Mwangesi katika hotuba yake amebainisha kuwa mafunzo hayo ni nguzo kuu kwa Watumishi hao katika kufanya kazi kwa bidii na kwa uadilifu mkubwa katika Utumishi wa Umma.
‘’Kila mmoja wenu anatakiwa kuzingatia mafunzo haya ,kwani ndio msingi katika Utumishi wa Umma na utakupelekea kufanya kazi kwa ufanisi na kwa viwango vilivyokusudiwa hadi utakapohitimisha Utumishi wako.’’ Alisisitiza
Awali akitoa neno la utangulizi Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Bi. Teddy Njau amesema kuwa mafunzo hayo ya siku tatu yanalenga kuwafanya Watumishi hao kujua Kanuni na Sheria za Utumishi wa Umma katika kutekeleza majukumu yao.
“Mafunzo haya ni muhimu kwenu katika kufanya kazi na ni matumaini yangu baada ya mafunzo hayo kila mmoja wetu atakua amepata kitu na hatimaye kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni na Sheria zilizopo katika utumishi wa Umma.’’ alisema.
Mafunzo haya ya siku tatu yamewashirikisha watumishi wapya kutoka katika ofisi zote za kanda pamoja na Makao Makuu.