Watumishi wa Umma watakiwa kukemea vitendo vya ufunjifu wa Haki za Binadamu.
Watumishi wa Umma wametakiwa kukemea vitendo vya ukiukwaji wa Maadili, Rushwa na uvunjifu wa Haki za Binadamu wanapotekeleza majukumu yao ili kuleta ufanisi katika kutoa huduma bora kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu Mhe Jaji (Stahiki) Mathew Mwaimu katika kongamano la kilele cha maadhimisho ya siku ya Maadili na Haki za Binadamu lililofanyika jijini Dodoma katika Ukumbi wa PSSSF tarehe 10 Desemba 2024.
“Lengo kuu la kongamano hili ni kutoa fursa kwa watumishi wa Umma kujitathimini namna wanavyotoa huduma kwa wananchi kwa kuzingatia Maadili na Haki za Binadamu na jinsi wanavyoweza kuepuka vitendo vya Rushwa wanapotekeleza majukumu yao “alisema.
Aidha Mhe, Mwaimu amewaasa watumishi wa Umma kutumia kongamano hili pamoja na mada zitakazotolewa kuepuka vitendo sivivyo vya kimaadili na vya ukiukwaji wa Haki za Binadamu wanapotoa huduma kwa wananchi ambavyo ni pamoja na Rushwa, unyanyasaji, dharau, kejeli na maringo na kwamba havitakiwi katika utumishi wa Umma.
Mhe. (Jaji) Mwaimu katika hotuba yake pia aliwataka viongozi wa Umma kufanyia kazi malalamiko yaliyotolewa na wananchi wakati wa uchaguzi wa Serikali za mitaa wa 2024 ili yasijirudie katika Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2025.
Mhe Mwaimu amefafanua kuwa vitendo vya uvunjifu wa Amani kwa wananchi pamoja na ukiukwaji wa Haki za Binadamu ni kosa kubwa na kwamba halitakiwi kufumbiwa macho.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni Tumia haki yako ya kidemokrasia chagua Viongozi waadilifu na wanaozingatia haki za binadamu na misingi ya utawala bora kwa maendeleo ya Taifa.
Mada mbili zimewasilishwa na kujadiliwa katika kongamano hilo ambazo ni Haki za binadamu katika mapambano dhidi ya Rushwa na mada ya pili niMaadili, Haki na wajibu wa watumishi wa Umma.
Maadhimisho ya siku ya Maadili na Haki za Binadamu kitaifa yameratibiwa na Taasisi zinazosimamia Utawala Bora nchini ambazo ni Ofisi ya Rais Ikulu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Wizara ya Katiba na Sheria, Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi, Tume ya Utumishi wa Umma, Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi, Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali pamoja na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.