Watumishi wa Umma waaswa kuepuka Vitendo vya Rushwa na kuzingatia Maadili na Haki za Binadamu.

Katika kuadhimishisha Siku ya Maadili na Haki za Binadamu nchini, Watumishi wa Umma wameaswa kuepuka vitendo vya rushwa na kuzingatia maadili na haki za Binadamu wakati wanapotoa huduma kwa umma.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Godfrey Mizengo Pinda (Mb) ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Duniani ambapo kwa hapa nchini yaliadhimishwa tarehe 10 Desemba, 2021 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Pinda alisema kuwa Watumishi wa Umma wanatekeleza majukumu yao kwa niaba ya Rais kwa mujibu wa Ibara ya 35 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
“Mtumishi akila rushwa au akikiuka haki za banadamu ni fedheha kwa Serikali na kwa jamii kwa ujumla, hivyo mtumishi huyo hastahili kuendelea na utumishi wake.” Alifafanua Mhe. Pinda.
Kwa upande wa wananchi, Mhe. Pinda alitoa rai kuwa kila mmoja wetu kwa nafasi yake atekeleze wajibu wake wa kutotoa wala kupokea rushwa kwani kutoa rushwa na kupokea rushwa yote ni makosa na hakutakuwa na rushwa endapo mtoa rushwa au mpokea rushwa asipokuwepo, alibainisha Mhe. Pinda.
Kuhusu Haki za Binadamu, Mhe. Naibu Waziri Pinda alisema kuwa Serikali imebeba kwa uzito wake suala la haki za binadamu na ndio sababu ilifikia uamuzi wa kuzifanya haki za binadamu kuwa sehemu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania – kama ilivyoanishwa katika Sehemu ya Tatu ya Katiba – kuanzia Ibara ya 12 – 24.
“Ni muhimu wananchi wote tukafahamu haki zetu lakini pia na wajibu wetu kama wananchi kwani hakuna haki bila wajibu.Wajibu wetu kama raia umefafanuliwa kuanzia Ibara ya 25 – 28 ya Katiba yetu.Ni vema kila mmoja wetu akasoma na kuzingatia haya kwa ustawi wa Taifa letu.” Alisisitiza Mhe. Pinda.
Kwa upande mwingine, Mhe. Pinda alitumia fursa hiyo kuwatahadharisha watanzania kuhusu janga hatari la ugonjwa wa UVIKO 19 ambapo alisema kuwa sote tunajua kuwa Dunia bado iko katika vita dhidi ya janga hilo ambalo halichagui nchi.
“Nawasihi Watanzania wenzangu tuungane na Serikali yetu katika kuhakikisha kuwa tunachukua tahadhari zote muhimu ikiwa ni pamoja na kupata chanjo, kutumia vitakasa mikono, kunawa kwa maji tiririka na kutumia barakoa pale ambapo tutakuwa kwenye mikusanyiko” alimaliza kusema Mhe. Pinda.
Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu kitaifa mwaka huu yalifanyika katika Viwanja vya Mnazi mmoja Jijini Dar es Salaam ambapo kauli mbiu ya maadhimisho hayo ilikuwa ni “Zingatia Maadili, Piga Vita Rushwa, Heshimu Haki za Binadamu ili kuimarisha Utawala Bora”.