Watumishi wa Sekretarieti ya Maadili Ya Viongozi wa Umma wametakiwa kuwajibika katika kutimiza majukumu yao.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe, Jenista Mhagama ametoa wito kwa watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kutekeleza jukumu lao la msingi la kikatiba la kufuatilia tabia na mienendo ya viongozi, kwa weledi, umakini, busara, na kwa uadilifu wa hali ya juu.
Mheshimiwa Mhagama ametoa kauli hiyo, katika Mkuatano wa Baraza la Wafanyakazi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma uliofanyika tarehe 24 mwezi Machi 2023, katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Dodoma.
Aidha, Mheshimiwa Mhagama katika hotuba yake alisema,” mnaposikiliza malalamiko ya wananchi dhidi ya viongozi wa umma na myafanyie kazi kwa uadilifu wa hali ya juu,” alisisitiza.
Mheshimiwa Mhagama alibainisha kuwa,wapo baadhi ya viongozi wa umma wanaojihusisha na vitendo vya mgongano wa maslahi wanapotimiza majukumu yao na wapo wengine ambao wanakinzana na wenzao hasa katika halmashauri zetu, hivyo Sekretarieti haina budi kufuatilia kwa karibu vitendo hivyo.
Mhe, Mhagama aliongeza kuwa, Sekretarieti ya Maadili ya viongozi wa umma inatakiwa kutoa elimu ya maadili kila inapopata nafasi ili dhana ya uadilifu na utawala bora ieleweke vizuri kwa viongozi na wananchi.
Amewataka watumishi wa Sekretarieti kutumia mbinu za uchunguzi kufuatilia kwa ukaribu viongozi wanaojihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili ikiwemo rushwa na mgongano wa maslahi ili haki iweze kutamalaki na kwale watakaobainika kukengeuka misingi ya maadili na utawala bora, taratibu na sheria za nchi zichukue mkondo wake.
Awali, Kamishna wa Maadili Mhe, Jaji Sivangilwa Mwangesi katika hotuba yake alifafanua kuwa, kikao hiki cha Baraza la wafanyakazi ni utekelezaji wa Waraka wa Rais namba 1 wa mwaka 1970 wenye maelekezo mahsusi kwa Taasisi za umma kuwa na mabaraza ya wafanyakazi kwa lengo la kuleta tija na ufanisi mahala pa kazi.
Mhe, Kamishna aliongeza kuwa, katika mkutano huu lengo ni kupata mawasilisho ya namna shughuli za Taasisi zilivyotekelezwana wajumbe kupata fursa ya kujadili na kutoa maoni kwa lengo la kuijenga Taasisi.
Mhe, Mwangesi alifafanua kuwa , pamoja na changamoto ambazo Taasisi inakabiliana nazo lakini bado kwa kutumia raslimali zilizopo Taasisi inatekeleza majukumu yake kwaweledi, uadilifu na ufanisi mkubwa na kutoa mchango wetu katika ustawi wa Taifa letu.
Katika hotuba yake Mhe, Mwangesi amewataka watumishi wote kutekeleza majukumu ya Taasisi tuliyokabidhiwa kisheria bila kupoteza uelekeo ili kufikia Dira yetu ya “Kuwa Taasisi yenye Ufanisi na Kuaminika katika kukuza na Kusimamia Misingi ya Maadili ya Viongozi wa Umma” na kwamba hilo linawezekana kwa kuwa tutaendelea kuwa waaminifu, waadilifu, wawajibikaji kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu.