WATUMISHI WA SEKRETARIETI YA MAADILI WAMETAKIWA KUTUMIA TEKNOLOJIA KATIKA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAO.
Watumishi wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa weledi unaoendana na matumizi ya teknolojia kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kamishna wa Maadili, Mhe. Jaji (Mst.) Sivangilwa Mwangesi alitoa agizo hilo alipokuwa akifungua kikao cha Baraza la wafanyakazi kilichofanyika katika ukumbi wa Ngorongoro jijini Arusha tarehe 20 Machi 2024.
“Fanyeni kazi kwa weledi na ubunifu unaoendana na kasi ya teknolojia na maendeleo ya Dunia huku mkizingatia sheria, kanuni na miongozo mbalimbali inayotolewa na viongozi wenu.” alisema,
Aidha, Mhe. Mwangesi katika hotuba yake ya ufunguzi aliwataka wajumbe wa Baraza la wafanyakazi kushiriki kikamilifu katika kujadili na kujipima utendaji wao wa kazi ili kuendelea kutoa huduma bora kwa uwazi, ufanisi na tija inayokidhi maslahi mapana ya Watanzania na Taifa kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Mhe. Mwangesi alieleza kuwa Sekretarieti ya Maadili imefanya kikao hicho cha Baraza la wafanyakazi ili kuzingatia agizo la Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la mwaka 1970 na ni utekelezaji wa kifungu cha 73(1-3) cha sheria Na. 6 ya mwaka 2004 ya ajira na mahusiano kazini kinachoelekeza kutekeleza sera ya ushirikishwaji wa wafanyakazi katika uamuzi wa pamoja
“Baraza la Wafanyakazi ndilo jukwaa la kisheria la majadiliano ya pamoja, kati ya menejimenti na watumishi mahala pa kazi kujadili masuala mbalimbali yanayowahusu wafanyakazi na waajiri wao, kwa lengo la kuhakikisha waajiri na watumishi wanatambua wajibu na haki zao, kuzingatia Sheria, Kanuni na maadili ya utumishi wa Umma kuleta matokeo chanya ya utendaji kazi wenye tija kwa taasisi na Taifa kwa ujumla,” alisema.
Kwa upande wake Katibu wa TUGHE mkoa wa Dodoma Bw. Samwel Nyungwa alisema, vyama vya wafanyakazi sio adui dhidi ya timu ya Menejimenti ila vipo kwa ajili ya kutoa ushirikiano mzuri kati ya wafanyakazi na uongozi, kitu ambacho sisi TUGHE tumefuraishwa na jinsi tawi letu la Sekretarieti ya maadili ya Viongizi wa Umma linavyopata ushirikiano na tunaomba ushirikiano huu uendelee.
Mwenyekiti wa tawi la TUGHE, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Bw. Mahina Henjewele aliupongeza uongozi wa Taasisi kwa kutoa uhuru pale shughuli za tawi zinapofanyika na kuhitaji msaada wa mwajiri.
“Naomba kutoa shukrani kwa uongozi wa Taasisi ambao wakati wote umekuwa ukitoa ushirikiano wa kufanikisha shughuli za tawi,” alisema.
Kikao hicho cha Baraza la wafanyakazi kiliwashirikisha viongozi kutoka makao makuu ya chama cha wafanyakazi (TUGHE) Taifa, Mkoa na wajumbe kutoka katika ofisi za Kanda na makao makuu.