Watumishi wa Sekretarieti ya Maadili wahitimisha wiki ya Utumishi wa Umma kwa kutembelea kituo cha watoto yatima.

Baadhi ya Watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma makao makuu Dodoma wahitimisha wiki ya Utumishi wa Umma kwa kutembelea kituo cha kulelea watoto yatima cha Kijiji cha Matumaini kilichopo Jijini Dodoma na kukabidhi baadhi ya mahitaji mbalimbali katika kituo hicho.
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Maadili wakati wa kukabidhi mahitajihayo, Katibu Idara ya Usimamizi wa Maadili Bw. John Kaole alisema kuwa tumeguswa sana na kazi kubwa inayofanywa na kituo hicho kwa kuwatunza na kuwalea watoto hao yatima ndio maana tumekuja kuwatembelea ili tuzidi kuwatia moyo wa kuendelea kufanya kazi hiyo.
Bw. Kaole aliongeza kuwa Ofisi yetu ndiyo inayosimamia maadili na tunaamini kuwa Maadili yanaanzia katika ngazi ya familia na kazi inayofanywa na kituo hicho ni kuwalea watoto katika Maadili mema jambo litakalosaidia kupata Viongozi bora na wenye Maadili hapo baadae.“ Sisi tumeamua kuja kuwaona watoto hawa kwa sababu sisi tunasimamia maadili”alisema.
“Tunawapongeza sana Wasimamizi na walezi mnaosimamia kituo hiki kwani mnawalea watoto hawa kwa upendo, lakini zaidi ya yote mnawapatia mahitaji yao yote ya kijamii naya muhimu kama chakula, elimu ,afya na mengineyo kwani watoto hawa wanaonekana kuwa na afya njema na furaha ya hali ya juu ”alisema Bw. Kaole.
Kwa upande wake Msimamizi wa kituo hicho Fr.Vincent Boselli alisema kuwa kituo hicho kilianzishwa 17 Agosti 2002,baada ya janga la UKIMWI kuongezeka na kuwa kubwa na kusababisha vifo kwa wazazi wengi na kuacha watoto wao yatima bila msaada wowote. Hadi sasa kituo hicho kina jumla ya watoto mia na sitini (160)
Fr. Boselli alisema kuwa lengo la kuanzisha kituo hicho ni kuwapa matumaini watoto ambao waliachwa yatima baada ya wazazi wao kufariki na kukosa matumaini kuwa wanaweza kuishi tena
“Tuliona kuna haja ya kutafuta mahali pa kuwalea na kuwatunza watoto hao baada ya kukosa upendo kutoka kwa wazazi wao kwani mtoto anahitaji upendo hata kama wazazi wake hawapo duniani’’alisema.
Fr. Boselli alifafanua kuwa wao kama kituo kinachosimamiwa na Kanisa Katoliki hawabagui watoto kulingana na imani zao.”Sisitunapokeawatoto wa Imani na dini zote na kuwalea kulingana na imani zao na hatumlazimishi mtoto kubadili dini yake’’
Aidha Fr. Boselli alitoa wito kwa jamii kwamba watoto hao ni kama watoto wao walioko majumbanina wana mahitaji kama walivyo watoto wengine kwa ujumla hivyo jamii inapaswa iwachukulie kama watoto wao wenyewe kwa kuwatunza ili watoto kama hao waweze kuishi kwa matumaini.
Akitoa shukrani kwa Sekretarieti ya Maadili Makamu Mkurugenzi wa kituo hicho Sr. Suzana Maingu aliwashukuru watumishi hao kwa upendo mkubwa wa kuwatembelea na kujitoa kwa ajili ya watoto hao kwani si wote wenye moyo huo wa kuwakumbuka watoto kama hao.
“Napenda kuwashukuru sana kwani mngeweza kufanya mambo mengine lakini mkaona kuna haja ya kuja kuwaona watoto hawa walioko pembezoni nakutoa majitoleo yenu kila mmoja kwa nafsi yakekwa kweli huo ni ukarimu mkubwa sana Mungu awabariki sana,” alisema Sr. Maingu.
Matembezi hayo ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma ambayo ilianza tarehe 16 na kilele chake ni tarehe 23 Juni 2022.