Watumishi wa Sekretarieti ya Maadili waadhimisha wiki ya Utumishi wa Umma Kitaifa kwa kupanda miti.

Watumishi wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kaskazini - Arusha wameadhimisha wiki ya Utumishi wa Umma kwa kupanda miti katika shule ya Msingi Kijenge iliyopo katika Halmashauri ya Jiji la Arusha, mkoani Arusha mapema wiki hii
Watumishi hao wamepanda miti mbalimbali katika maeneo ya shule ya msingi Kijenge kwa kushirikiana na baadhi ya wanafunzi wa Klabu ya Maadili ya shule hiyo.
Akizungumza na wanafunzi hao, Katibu Msaidizi Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kaskazini Bi. Anna Mbasha aliwaasa wanafunzi kuwa waadilifu, na mfano wa kuigwa kwa kuwa na tabia njema.
“Nyinyi ni taifa la kesho, hivyo, mnatakiwa kujiepusha na vitendo vya utovu wa maadili kama kuchukua vitu vya wenzenu bila kuomba na msome kwa bidii ili muweze kufanya vizuri katika masomo yenu,” alisema.
Bi. Anna alitoa rai kwa wanafunzi hao kuhakikisha miti iliyopandwa inatunzwa vizuri ili baadaye wanufaike na matunda yake ambayo ni matunda, kivuli na usafi wa mazingira ya shule yao.
Awali akimkaribisha Katibu Msaidizi, Mwalimu Mlezi wa Klabu ya maadili shuleni hapo Bw. Mosses Mhando aliishukuru Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kaskazini kwa kufungua klabu ya Maadili katika shule ya Kijenge na kupanda miti mbalimbali katika eneo la shule lililotengwa kwa ajili ya Klabu ya Maadili.
“Tutahakikisha miti hii tuliyoipanda leo, yote inatunzwa vizuri na hatimaye itawasaidia wanafunzi kufaidi matunda yatakayotokana na miti hii ikiwemo kivuli, kupendezesha eneo la shule na kuhifadhi mazingira ya shule.” Alisema Bw.Mosses.
Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma Kitaifa yalianza tangu Juni 16, 2022 na kilele chake ni hadi Juni 23, 2022.