Watumishi wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Arusha Wakumbushwa kutopokea zawadi sizizoruhusiwa Kisheria.

Watumishi wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Arusha Wakumbushwa kutopokea zawadi sizizoruhusiwa Kisheria.
Watumishi wa Umma wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Arusha wametakiwa kutopokea zawadi zisizoruhusiwa kisheria.
Hayo yameelezwa na Bw. Adam Kuhanda Afisa wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kaskazini katika mafunzo maalum ya maadili kwa Watumishi wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Arusha.
Bw. Kuhanda alisema kuwa watumishi wa umma hawapaswi kupokea zawadi zisizoruhusiwa kisheria kwani kwa kufanya hivyo zinaweza kuwapelekea kujiingiza katika mgongano wa maslahi ambao unaweza kuathili utendaji wao wa kazi.
Katika mafunzo hayo mbayo msisitizo mkubwa uliwekwa katika maeneo nane (8) yanayohusu tabia na mienendo ya kimaadili ambayo watumishi wa umma wanapaswa kuyazingatia, Bw. Kuhanda aliyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na kutoa huduma bora; utii kwa serikali na kutoa huduma bila upendeleo.
Kwa mujibu wa Bw. Kuanda maeneo mengine ni kufanya kazi kwa uadilifu; kuwajibika kwa umma na kuheshimu Sheria na matumizi sahihi ya taarifa.
Akitoa ufafanuzi kuhusu kutoa huduma bora kwa wananchi, Bw. Kuhanda aliwaeleza watumishi hao kuwa mtumishi wa umma anapaswa pamoja na mambo mengine kuzifahamu vema na kuziheshimu kanuni za maadili, kuweka malengo halisi ya kazi ili kukuwezesha kufikia kiwango cha juu kabisa katika utendaji wako wa kazi; kuwa na ubunifu na siku zote kujibidiisha kuongeza viwango vya utendaji kwa kujiongezea maarifa na ujuzi.
Kuhusu kufanya kazi kwa uadilifu Bw. Kuhanda aliwaeleza watumishi kuzingatia mipaka ya madaraka yako na wasiyatumie kwa manufaa binafsi na kuwakandamiza wengine, kuepuka madaraka yao kupendelea marafiki au jamaa zao pamoja na kusimamia vizuri fedha na mali za umma walizokabidhiwa ikiwemo kuzuia uharibifu, ubadhirifu na upotevu.
Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imejiwekea utaratibu wa kuwajengea uwezo wadau wake hususani Viongozi na watumishi wa umma pamoja na wananchi kuhusu Maadili kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma pamoja na Mafunzo hayo hufanyika kila mwaka ili kuwajengea uwezo watumishi wa mamlaka hiyo ili waweze kufanya kazi zao kwa uadilifu na kuzingatia sheria.