Watumishi wa Maadili “Wapigwa Msasa” kuhusu mbinu za kiuchunguzi.

Watumishi wa Maadili “Wapigwa Msasa” kuhusu mbinu za kiuchunguzi.
Watumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma wamepewa mafunzo juu ya mbinu mbalimbali za kiuchunguzi.
Mafunzo hayo ya siku nne yalifanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Kilimo cha Sokoine mjini Morogoro.
Akifungua mafunzo hayo Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji wa Rufani Sivangilwa Mwangesi alisema kuwa mafunzo hayo yanayolenga kuwajengea uwezo Maafisa Uchunguzi wa taasisi katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku na yataboresha utendaji kazi wa taasisi.
Aidha Mhe. Mwangesi alisema kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuwajengea uwezo na kuwapa mbinu bora za kufanya chunguzi mbalimbali, ukusanyaji na uchambuzi wa vielelezo, namna bora ya kufanya mahojiano, uchunguzi kwa njia ya mtandao, uandishi wa taarifa ya uchunguzi na kuendesha kesi katika Baraza la Maadili.
“Mafunzo haya ni muhimu sana kwenu kwani yatawajengea uwezo na kuondoa ombwe ambalo limekuepo wakati wa kufanya mahojiano, uchunguzi, ukusanyaji wa vielelezo na uandishi wa taarifa za uchunguzi” alisema.
Katika hatua nyingine Kamishna wa Maadili aliongeza kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuwajengea uwezo wa kufanya uchambuzi na uchunguzi wa nyaraka za fedha pamoja na uhalifu unaoweza kufanywa kwa ulaghai katika miamala, mikopo, hundi na mambo mengine yanayohusiana na fedha kwa viongozi wa umma ambapo ni uvunjifu wa kimaadili.
Mada mbalimbali zitawasilishwa na wakufunzi tofauti ikiwa ni pamoja na namna ya kutambua na kudhibiti mgongano wa maslahi, na Kanuni zake, mbinu za uchunguzi, ukusanyaji na uchambuzi vielelezo na uchunguzikwa njia ya mtandao.
Mafunzo hayo yamefadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB).