Watumishi Sekretarieti ya Maadili watakiwa kuwa waadilifu wanapotekeleza majukumu.
Kamishna wa Maadili nchini Mhe. Jaji (Stahiki) Sivangilwa Mwangesi ametoa wito kwa watumishi wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kufanya kazi kwa kutegemeana na kushirikiana kwa maendeleo ya Taasisi na Taifa kwa ujumla.
Mhe. Mwangesi ametoa rai hiyo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi tarehe 16 Oktoba, 2025.
“Baraza hili ni jukwaa muhimu la kuimarisha ushirikiano baina yetu na ndio sehemu nzuri ya kujadiliana kwa uwazi kuhusu mafanikio, changamoto na mikakati ya pamoja ya kuboresha utendaji kazi wetu na njia pekee ya kufanikisha hili ni kufanya kazi kwa ushirikiano wa dhati,” alisema Jaji Mwangesi.
Aidha Mhe. Mwangesi amewakumbusha watumishi kuendelea kutekeleza majukumu kwa weledi na uadilifu wa kiwango cha juu kwa maslahi mapana ya Taifa.
“Ni vyema tukumbuke kuwa tumepewa dhamana ya kusimamia uadilifu nchini na sisi ndio taswira ya Taifa linapokuja suala la kusimamia maadili na uadilifu kwa Viongozi wa Umma nchini, hivyo ni vyema sisi wenyewe tuwe waadilifu wakati wa utendaji wetu,” alisisitiza.
Pia Mhe. Mwangesi ametumia kikao hicho kuwakumbusha watumishi wa ofisi hiyo umuhimu wa nidhamu, uwajibikaji, weledi na uaminifu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa maslahi mapana ya Taasisi na Taifa kwa ujumla.
Baraza hilo linafanyika kwa siku mbili na linajadili mambo mbalimbali ikiwemo Taarifa ya Utekelezaji wa majukumu kwa mwaka wa fedha 2024/25, mafanikio ya Taasisi, changamoto pamoja na utekelezaji wa matumizi ya bajeti ya mwaka 2025/26.