WATUMISHI SEKRETARIETI YA MAADILI WAPIGWA MSASA KUHUSU UCHUNGUZI WA KIDIGITALI.

Watumishi wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambao ni wachunguzi pamoja na watunza kumbukumbu wamepatiwa mafunzo maalum ya mbinu mpya za kiuchunguzi na utunzaji wa siri.
Akifungua mafunzo hayo yaliyofanyika mkoani Iringa tarehe 27 Januari,2025 katika ukumbi wa Mount Royal Hoteli, Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji (Mst) Sivangilwa Mwangesi alieleza kuwa kutokana na ukuaji wa Teknolojia ni dhahiri kuwa wachunguzi wanapaswa kuongezewa uwezo wa namna bora ya kufanya uchunguzi wa kidijitaji ili kuboresha ufanisi katika uchunguzi hususan katika matumizi ya Teknolojia za kisasa ambazo husaidia kupata taarifa nyingi kwa haraka na zenye usahihi.
“Katika mafunzo haya mtaweza pia kuongeza uelewa katika eneo la uchunguzi katika maeneo maalumu mathalan eneo linalozidi kukua la uchunguzi wa miamala ya kielektroniki hususan fedha za kidijitali” alisema.
Katika hatua nyingine Mhe. Mwangesi alieleza kuwa mafunzo hayo yatawasaidia watunza kumbukumbu kuelewa namna ya kuhifadhi taarifa za kiuchunguzi kwa usalama zaidi ili kupuka uvujaji wa taarifa hizo.
“Katika mafunzo haya, mtajifunza kuhusu utunzaji wa kumbukumbu kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu. Mtajifunza namna ya menejimenti ya kumbukumbu kwa mifumo iliyoanzishwa na Serikali kwa lengo la kuongeza tija na kuimarisha usalama na usiri wa taarifa nyeti” alisema.
Awali akitoa neno la utangulizi katika mafunzo hayo Katibu Idara ya Usimamizi Maadili kutoka Ofisi ya Rais Sekrtarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Bw. Kassim Mkwawa alieleza kuwa dhumuni kubwa la mafunzo hayo ni kuhakikisha kwamba watumishi hao wanakua na uelewa wa kutosha wa namna ya kufanya uchunguzi hususan katika miamala ya kielektroniki.
Bw. Mkwawa alieleza kuwa mafunzo hayo yataangazia mambo muhimu kama vile kutambua viashiria vya ukiukwaji wa maadili katika miamala ya kielektroniki, kutumia mbinu na zana za uchunguzi wa kidijitali, na kuelewa sheria zinazohusiana na ushahidi wa kielektroniki.
“Katika mafunzo haya tutajifunza mbinu kama vile kuhoji mashahidi kwa ufanisi, kufanya ukaguzi wa kina wa historia ya lalamiko, na kutumia zana za uchambuzi za kisasa zitakazosaidia kushughulikia malalamiko au masuala kuhusiana na miamala ya kielektroniki ambao kiuhalisia siyo rahisi kuchunguza iwapo hauna ujuzi na maarifa”,alisema.
Mafunzo hayo ya siku tano yatatolewa na wakufunzi kutoka Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma pamoja na wakufunzi kutoka Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa.