WATUMISHI SEKRETARIETI YA MAADILI WAASWA KUFANYA KAZI KWA WELEDI

WATUMISHI SEKRETARIETI YA MAADILI WAASWA KUFANYA KAZI KWA WELEDI
Watumishi wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma wamesisitiwa kufanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia maadili bila kuyumba au kuyumbishwa katika shughuli zao za kila siku.
Hayo yemesemwa na Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji (Stahiki) Sivangilwa Mwangesi wakati akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi ya Rais, Sekretareiti ya Maadili ya Viongozi uliofanyika Makao Makuu ya ofisi hiyo jijini Dodoma tarehe 12 Machi, 2025.
‘’Tusikubali kuyumba au kuyumbishwa na hatimaye kutolewa kwenye mstari, tuendelee kufuata misingi ya weledi na maadili katika utendaji kazi kwa kuepuka rushwa na kushinda vishawishi na tamaa nyinginezo,’’alisema Mhe. Mwangesi.
Jaji Mwangesi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo ameongeza kuwa kwa kukubali kuwa mtumishi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, basi ni lazima uwajibike kwa kuzingatia nidhamu, uaminifu, uwazi na kupendana.
"Kwa mara nyingine niwakumbushe kuwa tunatakiwa kuwajibika kwa kuzingatia nidhamu, uaminifu, uwazi na kupendana na yeyote atakayeenda tofauti na hayo, atakuwa si miongoni mwetu na hatutasita kuchukua hatua stahiki dhiki yake," alisisitiza Jaji Mwangesi.
Katika hatua nyingine Jaji Mwangesi amewakumbusha baadhi ya watumishi wenye changamoto za kiuadilifu na kuwakumbusha kuhakikisha kuwa wanakua mstari wa mbele katika kuzingatia uadilifu na kufanya kazi kwa uzalendo.
‘’Ninafahamu kuna baadhi yetu wana changamoto za kiuadilifu katika utendaji wao, lakini kwakuwa Taasisi yetu tunayoitumikia ni ya kimaadili basi hatuna budi kukumbushana kwa lengo la kujipa muda kujitathmini na kujirekebisha kwenye suala la uaminifu, nidhamu, kupendana pamoja na utii kwa mamlaka na viongozi waliopo juu yetu," aliongeza.
Aidha, Jaji Mwangesi amewataka wajumbe wa Baraza hilo kuwa mabalozi kwa watumishi wengine kwenye suala la ujazaji wa majukumu katika mfumo wa e-utendaji ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Serikali.