WATUMISHI BODI YA TUMBAKU WAPATIWA MAFUNZO KUHUSU SHERIA YA MAADILI

Watumishi wa Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB) wamepatiwa mafunzo kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na kutakiwa kufanya kazi kwa pamoja, kuzingatia uadlifu na nidhamu ili kutimiza malengo ya Taasisi yao.
Wito huo umetolewa na Katibu Msaidizi, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Bw. Fabian Pokela katika mafunzo yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Nyerere uliopo katika hoteli ya Gold Crest jijini Mwanza Agosti 14, 2025.
Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo watumishi wa Bodi ya Tumbaku nchini kutekeleza majukumu kwa kuzingatia viwango vya juu vya uadilifu, nidhamu na kutoa huduma bila upendeleo kwa kila mmoja.
“Uadilifu katika kutekeleza majukumu yetu ni chachu ya maendeleo kwa jamii yoyote ile, takriban nchi zote zilizofanikiwa, zimekuwa na viwango vya juu vya uadilifu katika kutimiza malengo yao,’’ alisema Bw. Pokela.
Aidha, Bw. Pokela amesisitiza kuzingatia utoaji bora wa huduma na muonekano mzima wa mtoa huduma kwa kuzingatia kanuni zilizowekwa ili kuepuka upendeleo na kutoa huduma chini ya kiwango ama kwa upendeleo.
“Katika kutoa huduma lazima tuzingatie huduma yenyewe, namna huduma inavyotolewa na unadhifu wa mtoa huduma mwenyewe. Mtoa huduma anatakiwa kuvaa kulingana na waraka wa mavazi wa mtumishi wa Umma, vigezo hivi lazima vizingatiwe kwa mtoa huduma yoyote ambaye ni mtumishi wa umma,’’ alisisitiza.
Awali akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi Mkuu wa TTB Bw. Stanley Mnozya alisema kuwa wao kama Bodi wameandaa mafunzo hayo kwa lengo la kuwakumbusha watumishi misingi ya maadili katika utumishi wa umma kwani ndio ufunguo katika kutekeleza majukumu ya kila siku.
“Tutahakikisha kila mwaka tunaandaa mafunzo ya namna hii kwa watumishi wetu maana mtumishi mwema lazima awe na maadili mema na kujali rasilimali za nchi kwanza kwa maendeleo ya Taasisi na Taifa kwa ujumla,” alisema Bw. Mnozya.
Mafunzo hayo ya siku mbili pia yana wakumbusha watumishi kuzingatia uadilifu, kuepuka vitendo vya kutoa na kupokea rushwa, nidhamu na kujali afya wakati wa utekelezaji wa majukumu yao. Jumla ya watumishi 73 wameshirikii mafunzo hayo.