WANANCHI WAKUMBUSHWA WAJIBU WAO WA KUKUZA NA KUSIMAMIA MAADILI.
Wito huo umetolewa kwa wananchi nchini kupinga na kukataa kila aina ya uovu katika jamii ikiwemo rushwa, uonevu, wizi, ubadhirifu wa mali za umma na ya watu binafsi.
Katibu Msaidizi, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kaskazini, Arusha Bw. Gerald Mwaitebele ametoa wito huo tarehe 20.2.2024 wakati akitoa mada ya Maadili ya Viongozi wa Umma kupitia kituo cha redio cha Arusha One FM kilichopo jijini Arusha.
Bw. Mwaitebele amesema, “Kila mwananchi anawajibika kukuza na kusimamia maadili nchini yakiwemo maadili ya Viongozi wa Umma.”
Kwa mujibu wa Katibu Msaidizi, ni wajibu wa wananchi kuisaidia Serikali kwa kutoa taarifa zitakazowezesha kuchukua hatua za kisheria na kinidhamu kwa watumishi wa umma wanaotumia vibaya madaraka kinyume na misingi ya Maadili.
Ameitaja baadhi ya misingi hiyo kuwa ni kutoa huduma bila upendeleo, kutowaonea watu, kuepuka vitendo vya rushwa na kutumia mali ya umma kwa maslahi yao binafsi.
”Elimu hii tunayoitoa inalenga kuhimiza uadilifu katika maeneo ya kazi kwani utamaduni wa maadili unapojengeka katika jamii unasaidia kupunguza vitendo viovu katika jamii kwa kuwakumbusha viongozi wa umma kuzingatia maadili na kuwafichua viongozi wanaotumia madaraka yao vibaya,”alisema.
Katika hatua nyingine Bw. Mwaitebele aliwataka wananchi kuchagua viongozi waadilifu katika chaguzi zijazo na kuelimisha wenzao kuhusu masuala ya maadili na utawala bora.
“Tunapoelekea katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni vyema wananchi kuzingatia sifa za mtu muadilifu katika jamii ili kupata kiongozi muadilifu,” alisema.
Amezitaja baadhi ya sifa hizo kuwa ni usikivu, kutenda haki, kufanya kazi kwa bidii, kuwa mwaminifu katika hali zote na kufikiria kwa umakini kabla ya kutenda jambo lolote.