Walimu watakiwa kuwa chachu ya kuimarisha maadili kwa wanafunzi
Sekretarieti ya Maadili kwa kushirikiana na wakuu wa shule pamoja na walimu wakuu wametakiwa kuhakikisha klabu za maadili zilizoanzishwa shuleni zinaendelea kuwa hai na kufanya kazi kwa ufanisi ili kusaidia kuimarisha maadili mema miongoni mwa wanafunzi.
Wito huo umetolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Dkt. Toba Nguvila, wakati akifungua mafunzo ya walimu walezi wa klabu za maadili kutoka Jiji la Arusha na Halmashauri ya Wilaya ya Meru, yaliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, tarehe 11 Novemba, 2026.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Nguvila amesema kuwa klabu za maadili zinapokuwa hai shuleni zitasaidia kuwajengea wanafunzi uelewa mzuri kuhusu elimu ya maadili kuanzia ngazi ya shule za msingi hadi vyuo vikuu.
Amesisitiza kuwa ni muhimu kuwajengea watoto msingi imara wa maarifa na maadili mema tangu wakiwa wadogo, kwani malezi wanayoyapata katika hatua za awali za maisha yana mchango mkubwa katika kuwajenga kuwa watu wema katika jamii.
“Unachoingiza ndani ya kichwa cha mtoto ndicho atakachokitoa, hivyo ni lazima tuanze kuingiza vitu vizuri vya maarifa katika vichwa vya watoto wetu ili baadaye wawe watu wema,” amesema Dkt. Nguvila.
Aidha, amesema kuwa kuna umuhimu wa kuwa na walimu wengi watakaoshiriki kufundisha na kusimamia elimu ya maadili katika shule na vyuo mbalimbali ili kuhakikisha klabu hizo zinaendelea kuwa hai na kutimiza malengo yake.
Ameonya kuwa jamii isipozingatia suala la maadili katika malezi na makuzi ya watoto, kuna hatari ya kuwa na kizazi kijacho kisichozingatia misingi ya maadili mema.
“Ni wakati wa kukumbushana ni wapi tumekosea katika suala la maadili kwa watoto wetu pamoja na sisi wenyewe, ili tusipotee zaidi,” amesisitiza Dkt. Nguvila.
Kwa upande wake, Katibu Msaidizi wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Kanda ya Kaskazini, Bw. Gerald Mwaitebele, amesema kuwa Serikali imeona umuhimu wa kuanza kutoa elimu ya maadili kwa watoto tangu wakiwa wadogo, badala ya kusubiri hadi wanapokuwa watu wazima na kushika nafasi za uongozi.
Amesema kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha vijana wanajengewa misingi imara ya maadili tangu wakiwa shuleni ili waweze kuwa viongozi bora na wenye kuzingatia maadili wanapofikia nafasi za uongozi.
“Ndiyo maana Sekretarieti ya Maadili imekuja na mwongozo wa uanzishaji wa klabu za maadili katika shule na vyuo, ili tuanze kuwaandaa vijana wetu kuwa viongozi bora tangu wakiwa katika umri mdogo,” amesisitiza Bw. Gerald Mwaitebele.
