Walimu Kondoa Mji wajengewa uwezo kuanzisha na kuendesha Klabu za Maadili shuleni
Walimu wa shule za msingi na sekondari za Halmashauri ya Mji Kondoa wamepatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kuanzisha na kuendesha klabu za maadili katika shule zao, ikiwa ni lengo la kujenga kizazi bora chenye maadili ili kupata viongozi bora na waadilifu.
Mafunzo hayo yaliyotolewa na Maafisa wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kati-Dodoma, yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Mji Kondoa tarehe 3 Novemba, 2026.
Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kondoa, Bw. Said Majaliwa, amewataka walimu hao kuzingatia mafunzo hayo ili kuwa mfano bora kwa wanafunzi na kuongeza kuwa watoto hujifunza maadili kupitia matendo ya watu wanaowazunguka.
"Maadili yanaanza na sisi kama watumishi wa Umma, kisha vijana wetu wanajifunza kupitia sisi, hivyo mafunzo haya ni muhimu kwetu nawaomba tusikilize kwa makini ili kupata uelewa zaidi,” alisema.
Kwa upande wake mwezeshaji kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kati-Dodoma Bi. Philipina Kobelo, amewasisitiza walimu kuhakikisha wanaanzisha klabu za maadili katika shule zao na kuzisimamia ipasavyo ili kujenga na kukuza uelewa wa maadili kwa wanafunzi.
“Mbali na kuwajengea wanafunzi uelewa sahihi kuhusu maadili, pia klabu hizi zinawasaidia katika kujieleza kwa uhuru kuhusu changamoto za kimaadili wanazokutana nazo katika mazingira ya shule na maisha ya kila siku,” alisema Bi. Philipina.
Klabu za maadili zinazoanzishwa katika Taasisi za elimu nchini zina lengo la kusimamia na kuhakikisha wanafunzi wanakua katika misingi ya maadili mema, huku zikisaidia kurithisha na kuendeleza maadili kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
