WALIMU WALEZI WA KLABU ZA MAADILI JIJINI ARUSHA WAPEWA MAFUNZO YA MAADILI:
Katibu Tawala mkoa wa Arusha Bw. Massaile Mussa amezitaka shule zote za msingi, sekondari na vyuo mkoani humo kufungua klabu za maadili kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais,Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kanda ya Kaskazini ili kuwajengea wanafunzi misingi ya maadili , uzalendo na moyo wa kupenda nchi yao tangu wakiwa ngazi ya chini.
Kauli hiyo, imetolewa na Katibu tawala wa mkoa wa Arusha alipokuwa akifungua mafunzo ya walimu walezi wa Klabu za maadili mkoani humo yaliyofanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari Arusha tarehe 26 Agosti 2024.
’’Lengo kuu la kuanzishwa kwa klabu hizi ni kuwa ngazi muhimu za kuelekea kwenye kiwango cha juu cha uadilifu kwanim tabia na mwenendo mwema uanzia chini kama msemo usemao mtoto umleavyo ndivyo akuavyo’’ alisema.
Ameongeza kuwa, Maadili yatasaidia kukuza maendeleo ya mkoa na kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi mkoani Arusha na pia klabu hizi zitasaidia kupunguza utoro shuleni, mimba za utotoni na vitendo viovu kwa watoto wetu.
Awali akiwakaribisha walimu walezi wa klabu hizo Katibu Msaidizi kanda ya Kaskazini Arusha Bw, Gerald Mwaitebele alieleza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo walezi wa klabu za maadili jinsi ya kufungua na kuendeleza Klabu za maadili katika maeneo yao ya kazi na kuwalea wanafunzi hao katika misingi ya maadili mema.
Mada zilizojadiliwa katika mafunzo hayo ni pamoja na Sheria ya maadili ya viongozi wa Umma, Majukumu ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Misingi ya Maadili katika sekta ya Umma na Mwongozo wa ufunguaji na uendeshaji wa kalabu za Maadili.
Mafunzo hayo, yaliwashirikisha jumla ya walimu walezi zaidi ya 50 kutoka katika shule za msingi, sekondari na vyuo vilivyopo Jijini Arusha.