MWANGESI: VIONGOZI JITOKEZENI KWENYE MAFUNZO YA MAADILI

Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji (Stahiki) Sivangilwa Mwangesi ametoa wito kwa Viongozi wa Umma nchini kujitokeza kwa wingi kushiriki mafunzo ya maadili awamu ya pili ambayo yataanza mwezi Novemba, 2025.
Wito huo umetolewa jijini Arusha tarehe 10 Oktoba, 2025 kwenye kikao maalum cha kupokea taarifa ya awali ya mafunzo ya Maadili kwa viongozi pamoja na kupokea mpango kazi wa mafunzo kwa awamu ya pili unaotarajia kuanza hivi karibuni.
“Mafunzo haya yatasaidia kupunguza mienendo mibaya kwa kada mbalimbali katika Utumishi wa Umma na pia itawasaidia Viongozi kuwa waadilifu hasa katika kufanya maamuzi kwa kufuata misingi ya sheria, kanuni na taratibu zilizopo katika Utumishi wa Umma,’’ alisema Jaji Mwangesi.
Aidha Jaji (Stahiki) Mwangesi ameziomba timu za wataalamu kutoka Sekretarieti ya Maadili pamoja na Chuo cha Uhasibu Arusha kujipanga vyema katika kutekeleza kikamilifu mpango wa mafunzo hayo kwa awamu ya pili ili kuwafikia Viongozi wengi na kuzidi kuimarisha Utawala Bora.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) Dkt. Grace Idinga amesema kuwa mafunzo ya awali yalikuwa na ufanisi mkubwa na Viongozi waliyapenda na waliomba kuwepo na mkakati wa kuwafikia Viongozi wengi hasa wa chini kama Wakuu wa Idara na Vitengo.
“Katika awamu ya kwanza kuna makundi ya Viongozi hatukuwafikia hivyo awamu hii tumepanga tuwafikie kwa idadi kubwa hasa wale wa chini kama vile Wakuu wa Idara, Wakuu wa Vitengo, Wenyeviti wa Halmashauri pamoja na kamati zao,” alisema, Dkt. Idinga.
Aidha Dkt. Idinga ameongeza kuwa kama kuna Taasisi ambayo itakua tayari kwa kuwaweka pamoja viongozi wao kwa ajili ya kupata mafunzo hayo, fursa hiyo ipo wazi na wao watakua tayari kufika popote kwa ajili ya kutoa mafunzo hayo.
Mnamo Machi, 2025 Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma na Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) walizindua hati ya makubaliano ya kukuza maadili kwa Viongozi wa Umma ambapo awamu ya kwanza ilifanyika Mei na Juni, 2025 na kwa sasa mpango wa mafunzo hayo kwa awamu ya pili unatarajia kuanza Novemba, 2025 ukiwa na lengo kuu la kuboresha utoaji wa huduma kwa jamii nchini.