Wito watolewa kwa watumishi Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuzingatia weledi, uadilifu na ushirikiano
Kamishna wa Maadili, Mhe. Jaji (Stahiki) Sivangilwa Mwangesi, amewataka watumishi wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu, bidii na ushirikiano ili kuiwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake pamoja na kufikia malengo ya Taasisi.
Mhe. Mwangesi ametoa rai hiyo wakati akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Royal Tughimbe jijini Mbeya, Oktoba 22, 2026.
Katika hotuba yake, Mhe. Mwangesi amesisitiza kuwa kila mtumishi anapaswa kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma, huku akiepuka uzembe, uvivu na mazoea yanayoweza kukwamisha utekelezaji wa majukumu ya Serikali.
“Tumepata dhamana ya kuiwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake, hivyo rai yangu kwenu ni kuendelea kutekeleza majukumu mliyonayo kwa weledi na uadilifu wa kiwango cha juu, kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa letu,” alisema Mhe. Mwangesi.
Aidha, Mhe. Mwangesi amesisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa ubunifu, kujituma na kutunza siri za Serikali na kuzingatia kuwa mafanikio ya Taasisi yanategemea mchango wa kila mmoja.
“Katika kutekeleza majukumu yetu ni vyema kuwa wabunifu, wenye kujituma na kuzingatia utunzaji wa siri za Serikali, pamoja na kufuata maelekezo kutoka maeneo mbalimbali kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu,” alisema Mhe. Mwangesi.
Katika hatua nyingine Mhe. Mwangesi amewataka watumishi wa ofisi hiyo kutumia nafasi zao kikamilifu, kufanya kazi kwa bidii na kushirikiana katika kutekeleza majukumu yao, ili Taasisi hiyo iweze kutimiza dhamana yake kwa Serikali na Taifa kwa ujumla.
