Walezi wa Klabu za Maadili waswa kuwa na maadilii

Baadhi ya walezi wa klabu za maadili ambao ni waalimu kutoka shule za Sekondari na Msingi katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma wamepatiwa mafunzo kuhusu maadili. Mafunzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa shule ya Sekondari Dodoma tarehe 28 Oktoba, 2022.
Akifungua mafunzo hayo Kaimu Katibu Msaidizi Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya kati –Dodoma Bi. Modesta Mtui alisema kuwa walezi wa Klabu za maaadili wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuwa na maadili mema kwani mtoto anachokiona ndicho atakachokiishi hivyo mwalimu yeyote ni kioo kwa wanafunzi wake “Ni ngumu sana kwa mwalimu ambaye hana maadili kumfundisha mwanafunzi kuwa na maadili mema na mwanafunzi akaelewa’’’alisema.
Bi. Modesta alisema kuwa lengo la mafunzo hayo kwa walezi wa klabu hizo ni kupata uelewa wa pamoja juu ya dhana panaya maadili ili walezi hao wa klabu za maadili wawasaidie wanafunzi kuyaishi yale wanayofundishwa jambo litakalo wasaidia kuwa waadilifu toka utotoni hata watakapokua wakubwa.
Bi. Modesta alieleza kuwa Serikali kupitia Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambacho ndio chombo kikuu cha usimamizi wa maadili ya Viongozi nchini , iliona ni vyema kueneza maadili kwa wanafunzi walioko ngazi mbalimbali za masomo kama vile shule za msingi, sekondari pamoja na vyuo vikuu kwa kuanzisha klabu za maadili ikiaminika kuwa tabia na mienendo mwema kwa binadamu hufundishwa tangu akiwa mdogo na hasa akiwa shuleni au chuoni.
Aidha Bi. Modesta alisema kuwa Lengo la kuanzishwa kwa klabu za maadilini kuwajengea wanafunzina wanavyuo misingi bora ya maadili tangu wakiwa Shuleni na Vyuoni. Klabu hizo pia zitasaidia kuwatengeneza mabalozi wazuri wa Sekretarieti ya Maadili watakaosaidia kueneza na kuelimisha familia zao kwa ujumla juu ya suala la maadili. Klabu hizo pia zitawasaidia wanafunzi kujitambua na kujipambanua kitabia na kuachana na mienendo isiyofaa.
Akibainisha changamoto wanazokutana nazo walezi wa klabu za maadili ambao ni waalimu wa shule mbalimbali Mwalimu Marcus Magwa ambaye ni mlezi wa klabu ya maadili katika Shule ya Sekondari Dodoma alisema kuwa kutokana na kukua kwa utandawazi kwa sasa watoto wengi wanapata misukumo ya mienendo mibaya kutoka kwenye mitandao jambo linalowafanya watoto hao kuona kuwa kuwa na maadili ni ushamba mfano katika suala la mavazi mtoto anaona kuvaa nguo zinazomstiri mwili wake ni jambo lililopitwa na wakati.
Aidha Mwalimu Marcus alitoa wito kwa wazazi kutenga muda wa kukaa na watoto wao na kufuatilia mienendo yao ili kuweza kubaini mapema iwapo mtoto ana mienendo isiyofaa ili washirikiane na waalimu kuweza kudhibiti hali hiyo mapema .
Pamoja na hayo Mwalimu Marcus alitoa rai kwa Sekretarieti ya Maadili kuongeza kasi ya kueneza maadili nchini hususan kutoa elimu ya mara kwa mara kwa wanachama wa klabu ya maadili ili kuendana na kasi ya ukuaji wa utandawazi nchini ’’ utandawazi una nguvu unakua kwa kasi sana’’ alisema.
Katika mafunzo hayo walezi wa klabu za maadili watapata uelewa wa pamoja juu ya shughuli zinazotekelezwa na Sekretarieti ya Maadili, majukumu ya Sekretarieti ya Maadili .Katika mafunzo hayo walezi wa klabu za maadili watapata fursa yakupitia mwongozo wa kuanzisha na kuendesha klabu za maadili katika shule za msingi, Sekondari na Vyuo vya elimu Tanzania na kutoa maoni yao juu ya namna bora yautekelezaji wa mwongozo huo.