WAKUU WA WILAYA WAPYA WATAKIWA KUHESHIMU NA KUVIISHI VIAPO VYAO

Katibu Msaidizi wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kati Dodoma Bibi Jasmin Awadh i amewataka Wakuu wapya wa Wilaya walioteuliwa hivi karibuni kuheshimu na kuviishi viapo vyao walivyoviapa kwa uadilifu na uaminifu mkubwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Bibi Awadhi alitoa kauli hiyo alipokuwa akiongoza kiapo cha Ahadi ya Uadilifu kwa Mkuu wa wilaya ya Chemba Mhe. Gerald Lomward Mongela katika hafla fupi iliyofanyika katika ukumbi wa Ofis i ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma tarehe 30 Januari 2023.
Alisema, “hakikisheni mnajitoa kutumikia viapo mlivyotoa mbele yetu na kuviweka katika kumbukumbu zenu za kila siku ili viwasaidie kuyakumbuka yale yote yaliyoelezwa katika viapo hivyo mnapotekeleza majukumu yenu ya kila siku.”
Katika hatua nyingine Bibi Awadhi alimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Chemba kwa kuteuliwa kwake na alisema kuwa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekupa heshima kubwa ya kuiongoza wilaya ya Chemba.
Katibu huyo Msaidizi pia aliwapongeza wakuu wengine wapya wawila ya za Bahi Mhe. Godwin Gondwe na Mpwapwa Mhe. Sophia Kizigo waliohamishiwa mkoani Dodoma katika mabadiliko ya vituo vya wakuu wa wilaya yaliyofanyika hivi karibuni.
Awali Mhe. Rosemary Senyemule Mkuu wa Mkoa wa Dodoma alimwapisha Mhe. Gerald Lomward Mongela kuwa Mkuu wa wilaya ya Chemba, hafla hiyo pia iliudhuriwa na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Dodoma wakiwemo Viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa, Kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa pamoja na Manejimenti ya ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Dodoma.