Wakuu wa Vitengo na Idara za TEHAMA wajengewa uwezo matumizi ya ODS
Wakuu wa Vitengo na Idara za TEHAMA kutoka Taasisi za Umma na Wizara nchini wametakiwa kuwa msaada kwa kuwaelekeza Viongozi wengine katika Taasisi zao namna ya matumizi ya mfumo wa ujazaji Tamko la Rasilimali na Madeni kwa njia ya Mtandao (Online Declaration System-ODS).
Rai hiyo imetolewa na Katibu Msaidizi Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kati-Dodoma Bi. Jasmin Awadhi wakati akifungua mafunzo ya maadili kwa Wakuu wa Vitengo na Idara za TEHAMA kutoka Taasisi za Umma na Wizara yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi jijini Dodoma tarehe 03 Machi, 2026.
“Lengo la mafunzo haya ni kuwapitisha katika matumizi ya mfumo wa ujazaji Tamko la Rasilimali na Madeni kwa njia ya Mtandao na baada ya kupata uelewa wa mfumo huu tunatarajia mtakua msaada kwa wengine katika kujaza Tamko,”alisema.
Aidha Bi. Jasmin ameongeza kuwa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma haijakataza Kiongozi kumiliki mali, bali ni nyenzo katika kuhakikisha kuwa Viongozi wa Umma wanapata mali zao kwa njia halali kwa kuepuka matumizi mabaya ya madaraka na magongano wa maslahi.
“Sheria hii haimzui mtu kuwa na mali kwa kadri alivyojaliwa ila katika kulinda taswira ya Kiongozi na Serikali kwa ujumla, Kiongozi lazima atafute mali zake kwa njia sahihi na kisha kuzitamka kwa mujibu wa Sheria,” alisisitiza Bi. Jasmin.
Awali akitoa mada kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Afisa Maadili kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Kati-Dodoma Bw. Anno Mgani amesema kuwa Kiongozi mzuri ni yule anayefanya kazi kwa kuzingatia weledi, mwenye kuepuka kuomba au kupokea fadhila yoyote ya kiuchumi na mwenye kutoa huduma bila upendeleo.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA kutoka Chuo cha Mipango na Maendeleo Vijijini Bw. Jabir Saleh Abdi amesema kuwa mafunzo hayo ni mazuri kwani matumizi ya mfumo wa ODS yameondoa matumizi ya karatasi ngumu ambapo gharama kubwa ilikua ikitumika katika kujaza na kuwasilisha Tamko la Rasilimali na Madeni kwa Kamishna wa Maadili.
“Mfumo umeleta nafuu katika kujaza taarifa zetu, kwani unafanya kazi popote penye huduma ya mtandao, hivyo ni rahisi kwetu kujaza Tamko tukiwa ofisini bila kuathiri utekelezaji wa majukumu yetu ya kila siku,” alisema Bw. Abdi.
Mafunzo hayo yaliyowashirikisha Wakuu wa Vitengo na Idara za TEHAMA kutoka Taasisi za Umma na Wizara yalikua na lengo la kuwajengea uwezo Viongozi hao katika matumizi ya mfumo kwenye kujaza Tamko la Rasilimali na Madeni kwa njia ya Mtandao (Online Declaration System-ODS) na wao kutakiwa kuwa mabalozi wazuri wa mfumo huo kwa Viongozi wengine katika maeneo yao ya kazi.
