Wakurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu wajengewa uwezo juu ya Sheria ya Maadili ya Maadili ya viongozi wa Umma.
Wakurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu kutoka kaika Wizara na Taasisi mbalimbali za umma wamejengewa uwezo juu ya Sheria ya Maadili ya Maadili ya viongozi wa umma sura ya 398 [marejeo ya 2023]. Mafunzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa Zabibu Hotel Mkoani Dodoma tarehe 29 Aprili, 2026.
Akifungua mafunzo hayo Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji (Stahiki) Sivangilwa Mwangesi alisema kuwa Ofisi yake imeandaa mafunzo mahsusi kwa Wakurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu kwa lengo la kuwajengea uelewa wa kina kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma pamoja na kuwapa ujuzi wa namna ya kutumia Mfumo wa Kielektroniki wa Uwasilishaji wa Matamko ya Mali na Madeni kwa njia ya mtandao.(Online Declaration System – ODS).
“Mafunzo haya yameandaliwa mahsusi kwa ajili yenu, kwa kutambua nafasi yenu ya kipekee katika kusimamia rasilimali watu ndani ya Taasisi za Umma, pamoja na jukumu lenu muhimu katika kuhakikisha utekelezaji wa misingi ya maadili katika utumishi wa umma” alisema.
Katika hatua nyingine Mhe. Jaji alisisitiza suala la Maadili kwa Viongozi wa Umma na kusema kuwa Maadili yanaanza na Kiongozi mwenyewe “Maadili siyo jambo la ziada katika utumishi wa umma, Bila maadili, hakuna uaminifu; na bila uaminifu, hakuna Utawala Bora” alisema.
Aidha Mhe. Mwangesi katika hotuba yake aliwakumbusha viongozi hao juu ya wajibu wao wa kisheria wa kutoa matamko ya Raslimali na madeni ndani ya muda uliowekwa ambapo kwa sasa Viongozi hao wanatoa matamko hayo kwa njia ya mtandao.
“Kama mnavyofahamu, mfumo huu wa kujaza matamko kwa njia ya mtandao ODS umeanzishwa ili kuboresha uwazi, ufanisi na urahisi katika utekelezaji wa matakwa ya kisheria ya utoaji wa matamko. Kupitia mfumo huu, viongozi wa umma wanaweza kuwasilisha taarifa zao kwa njia ya kisasa, salama na inayorahisisha ufuatiliaji na uhakiki”alisema.
Mhe Mwangesi pia aliwasisitiza viongozi hao kutoa taarifa kwa wakati kwa Sekretarieti ya Maadili kuhusu watumishi wote wanaoteuliwa au kupandishwa vyeo na kuingia katika nafasi za uongozi wa umma ili kuwezesha usajili wa viongozi hao katika mifumo ya Sekretarieti, hususan mfumo wa ODS na kuwaelekeza viongozi hao juu ya wajibu wao wa kisheria wa kutoa matamko ndani ya muda uliowekwa, na kusimamia ufuatiliaji wa utekelezaji wa wajibu huo ndani ya taasisi zao.
Mada mbili ziliwasilishwa katika mafunzo hayo ikiwa ni mada kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma pamoja na mada kuhusu namna ya ujazaji wa Tamko la Rasilimali na Madeni kwa njia ya mtandao (ODS)
