Wajumbe wa Kamati ya Ukaguzi wapatiwa mafunzo kuhusu ukaguzi.

Wajumbe wa Kamati ya Ukaguzi na Menejimenti ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma wamepatiwa mafunzo kuhusu ukaguzi. Mafunzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma tarehe 20 Septemba,2022.
Akifungua mafunzo hayo Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi alisema kuwa katika kuhakikisha Kamati ya Ukaguzi inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, Sekretarieti ya Maadili imeandaa mafunzo hayo muhimu yatakayoshirikisha wajumbe wa kamati pamoja na menejimenti ili kuwa na uelewa wa pamoja katika namna bora ya uendeshaji na usimamizi wa Taasisi.
Mhe. Mwangesi alieleza kuwa Kamati ya Ukaguzi ina kazi muhimu sana ya kutoa ushauri kwa Afisa Masuuli kuhusu masuala ya uendeshaji wa Taasisi katika maeneo ya menejimenti ya vihatarishi, mifumo ya udhibiti na masuala ya utawala bora kwa ujumla.
Pamoja na hayo kamati ya ukaguzi inatoa ushauri katika masuala mbalimbali ya uendeshaji wa Taasisi hususani usimamizi wa fedha, rasilimali watu, shughuli mama za Taasisi, manunuzi na masuala mengine mengi jambo ambalo limeisaidia Taasisi kupata hati inayoridhisha ya ukaguzi.
Aidha Mhe. Mwangesi aliendelea kusema kuwa Kamati ya Ukaguzi kupitia ushauri wake inasaidia sana kuleta imani kwa wadau juu ya Taasisi inavyoendeshwa.
Mafunzo hayo ya siku mbili yatawapa washiriki fursa ya kufahamu namna shughuli kuu za Taasisi (Bussiness Process) zinavyofanyika na kuwawezesha washiriki kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi mkubwa