WAHESHIMIWA MAHAKIMU MKOA WA KILIMANJARO WAASWA KUJIEPUSHA NA MGONGANO WA MASLAHI


WAHESHIMIWA MAHAKIMU MKOA WA KILIMANJARO WAASWA KUJIEPUSHA NA MGONGANO WA MASLAHI
04
Sep
2023

Mahakimu wa mkoa wa Kilimanjaro wametakiwa kujiepusha na vitendo mbali mbali vinavyopelekea kuwepo kwa mgongano wa Maslahi.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Msaidizi kanda ya kaskazini Arusha Bi. Anna Mbasha alipokuwa akitoa mafunzo kwa mahakimu wa ngazi mbalimbali wa mkoa wa Kilimanjaro kuhusu maadili hivi karibuni.

Aidha, Bi. Mbasha alifafanua kuwa mgongano wa maslahi ni miongoni mwa matataizo ya kimaadili yanayozikumba nchi nyingi duniani na kwamba tatizo hili lina madhara makubwa kwa maendeleo ya nchi kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni lisipodhibitiwa.

“Mgongano wa Maslahi ni hali ya kukinzana kati ya maslahi binafsi ya kiongozi wa umma na kazi au majukumu yake kwa umma,” alisema.

Kwa mujibu wa Katibu huyo Msaidizi, maslahi binafsi yanaweza kuathiri utekelezaji wa majukumu ya Kiongozi kwa misingi ya haki na usawa, au upatikanaji wa ukweli.

Bi. Mbasha aliyataja mazingira yanayosababisha Mgongano wa Maslahi kuwa ni pamoja na Kudai, kuomba na kupokea zawadi, fadhila na maslahi ya kiuchumi yasiyostahili, kushindwa kutamka manufaa binafsi yanayoonekana moja kwa moja au vinginevyo katika Mkataba na Serikali pamoja na Matumizi ya rasilimali za umma kwa maslahi binafsi.

Mazingira mengine ni pamoja na matumizi mabaya ya magari ya umma, simu, kompyuta, kusaidia kampuni binafsi katika kupata kandarasi serikalini, kutumia muda wa saa za kazi kutekeleza shughuli za Kampuni binafsi na kushindwa kutamka maslahi binafsi katika mikataba na Serikali.

“Kiongozi wa Umma kutumia taarifa za utumishi wake uliopita kujinufaisha mwenyewe au kumsaidia mtu mwingine kupata manufaa binafsi, kupokea au kuomba fadhila au manufaakama vile usafiri, kulipiwa ada za shule, vitendo vyote hivi vinapelekea kuwepo kwa mgongano wa maslahi na pia ni ukiukaji wa Maadili kwa kiongozi wa Umma,” alisema.

Mafunzo haya ya Waheshimiwa Mahakimu yaliwashirikisha zaidi ya Mahakimu 60 wa ngazi mbali mbali wa mkoa wa Kilimanjaro.