JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA RAIS – SEKRETARIETI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA

Wahariri wa vyombo vya habari nchini wajengewa uwezo kuhusu majukumu na Mamlaka ya Sekretarieti ya Maadili
29 Aug, 2023
Wahariri wa vyombo vya habari nchini wajengewa uwezo kuhusu majukumu na Mamlaka ya Sekretarieti ya Maadili

Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini wamejengewa uwezo kuhusu mamlaka na majukumu yanayotekelezwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Mkutano huo wa kuwajengea uwezo ulifanyika katika Ukumbi wa Arnaoutoglou Jijini Dar es Salaam tarehe 17 June, 2023.

Akifungua mkutano huo Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji (Mst.) Sivangilwa Mwangesi alisema kuwa Vyombo vya habari vimekuwa na mchango mkubwa katika jamii na duniani kwa ujumla kwani vimeifanya dunia kuwa kama kijiji.

“Nikiri kwamba kusingekua na vyombo vya habari tusingejua mambo mengi yanayoendelea duniani. Leo hii unaweza ukakaa kwenye runinga yako, redio ama simu na ukapata habari kutoka ndani na nje ya nchi,” alisema.

Mhe. Kamishna aliwapongeza wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini kwa weledi wao katika utendaji wao wa kazi wa kila siku kwani wamekua mstari wa mbele kuielezea jamii mambo mengi na makubwa yanayofanywa na Serikali na kuibua changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi ili ziweze kutatuliwa na Serikali.

“Sote ni mashahidi tumeona namna mnavyotumia kalamu zenu katika kuwahabarisha wananchi juu ya shughuli zote zinazotekelezwa na Serikali yetu na pale mnapoibua changamoto za wananchi tumeona jinsi Serikali inavyozitatua kwa wakati,” alisema.

Aidha, Mhe Mwangesi alieleza kuwa dhumuni kubwa la Ofisi yake kukutana na wahariri hao ni kuwaelimisha namna Sekretarieti ya Maadili inavyofanya kazi, Majukumu na Mamlaka ya Sekretarieti ya Maadili kwa mujibu wa Ibara ya 132 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Kuifafanua kwa kina Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na.13 ya mwaka 1995 pamoja na kanuni zake na kuelezea misingi mbalimbali ya Maadili.

Kwa mujibu wa Mhe. Kamishna Taasisi yake inaamini kuwa iwapo wahariri wa vyombo vya habari wataelewa vizuri Majukumu na Mamlaka yake, ni dhahiri kuwa Umma wa Watanzania utahabarishwa kwa usahihi habari zinazohusu viongozi wa umma.

“Sekretarieti ya Maadili haiwezi kufanya kazi ya kusimamia tabia na mwenendo wa Viongozi wa Umma bila kuwashirikisheni nyinyi, tunawategemea muwajulishe wananchi majukumu yetu ili watuelewe, watupe ushirikiano na kutoa taarifa kwetu kuhusu ukiukwaji wa maadili,” alisema.

Aidha, Mhe. Mwangesi aliwashukuru wahariri kwa michango na maoni yao mazuri yaliyolenga kuboresha utekelezaji wa majukumu ya taasisi, na kwa kuitikia wito wa kuhudhuria mkutano huo.

“Nawashukuru sana kwa uvumilivu wenu, michango yenu mizuri na hii inaonyesha kuwa pande zote mbili zinahitajiana kwa maendeleo ya Taifa letu, naomba muwe mstari wa mbele kusema pale mnapoona ama kusikia kuhusu ukiukwaji wa maadili kwa Viongozi kwasababu Serikali yetu haiwezi kufikia malengo yake kama viongozi walioaminiwa na kupewa mamlaka ya kusimamia maendeleo watakosa uadilifu,” alisema.

Kwa upande wake Bw. Neville Meena, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), aliipongeza Sekretarieti ya Maadili kwa kuona umuhimu wa kukutana na wahariri wa vyombo vya habari nchini kwasababu kitendo hiki kitasaidia wahariri kuielewa vizuri Taasisi hii na kujenga ubia kati ya pande hizo mbili.

“Tunashukuru kwa uvumilivu wa Kamishna wa Maadili, kwa uwepo wake hapa kwetu umekuwa ni Baraka na neema. Kitendo hiki kinaifanya TEF kuingia ubia wa kuisemea Sekretarieti ya Maadili kwa wananchi.”

Kwa mujibu wa Bw. Meena, awali hawakujua ni wapi wawaelekeze wananchi kuwasilisha kero zao zinazotokana na baadhi ya viongozi wasio waadilifu.

“Wananchi sasa watajua mahali pa kusemea. Tusipokuwa na mahali pa kusemea tutajenga Taifa la watu wenye hasira,” alisema na kuongeza kuwa, “mawasilisho yenu yatatumika kama rejea na katika utendaji wetu wa kazi tutayatumia kutoa makala, ushauri na maoni.”

Katika mkutano huo, jumla ya mada mbili ziliwasilishwa. Mada hizo ni Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma pamoja na Ukuzaji wa Maadili.

Online Help
Kuanzisha Enzi Mpya katika Udhibiti wa Sekta ya Michezo ya Kubahatisha nchini Tanzania
Ofisi ya maadili inafanya kazi na imewashughulikia viongozi wengi sana kupitia Baraza la Maadili ambalo pia liliendeshwa mwaka 2013 Novemba mkoani Tabora. Viongozi mbalimbali waliokuwa na tuhuma za ukiukaji wa maadili waliitwa kwenye Baraza na kuhojiwa na Baraza linatoa mapendekezo na kuyawasilisha mapendekezo hayo kwa Rais kwa ajili ya hatua zaidi za kinidhamu na kisheria kwa viongozi husika.

" >
Kifungu cha 11(1) cha Sheria ya Maadili kimeainisha wazi mali zinazotakiwa kutajwa kuwa ni fedha taslimu, fedha zilizopo katika taasisi za kifedha kama vile benki, hisa, nyumba, mashamba, magari, mitambo na mali nyinginezo. Kiongozi anatakiwa kutoa tamko la mali anazomiliki yeye mwenyewe, mke/mume na watoto walio chini ya umri wa miaka kumi na nane. Fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni zinatakiwa kujazwa kila mwaka na kiongozi hutumiwa fomu hizo na Ofisi ya Maadili na pia zinapatikana katika mtandao wa maadili yaani www.ethicssecretariat.go.tz. Sheria inamtaka kiongozi kutolea tamko madeni yake ili kuweza kujua kuwa kiongozi anamiliki mali zipi na pia kutambua kuwa amezipata vipi mali hizo ukilinganisha na kipato cha kiongozi husika. Kiongozi kuwa na mali nyingi si dhambi kwani hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetamka wazi kuwa kila raia ana haki ya kumiliki mali ila ofisi inataka kujiridhisha uhalali wa jinsi mali ilivyopatikana. Mapendekezo katika Katiba mpya yanasisitiza maadili kwa kutenganisha uongozi na biashara.

" >
Wananchi wengi wamejijengea dhana kuwa bila pesa huwezi kupata huduma ya kiserikali kitu ambacho si kweli kwani huduma nyingi za kiserikali zinatolewa bure kabisa ila cha msingi wananchi wanatakiwa kutoa taarifa katika vyombo husika pindi wanapotakiwa kulipia huduma ambazo zinatolewa bure. Jamii inatakiwa kubadilika na kuamini kuwa si lazima kutoa rushwa ndipo upate huduma. Wapo wananchi wengi ambao walileta malalamiko kama hayo na Ofisi ya Maadili iliyashughulikia, hivyo wananchi wasisite kutembelea Ofisi zetu kwa ajili ya kutoa taarifa kama hizo.

" >
Kutoa lugha chafu ni ukiukwaji wa maadili. Ndani ya Bunge kuna Kamati ya Maadili ambayo ipo kwa ajili ya kuwawajibisha wabunge wanaotoa lugha chafu. Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa upande wake ilifanya semina kwa wabunge ili kuwakumbusha mipaka ya utendaji kazi na maadili kwa ujumla, na tangu wakati huo matumizi ya lugha chafu bungeni yamepungua kwa kiasi kikubwa.

" >