VIONGOZI WAASWA KUZINGATIA MAADILI

Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Reuben Shigella amewataka Viongozi wa Umma Mkoani humo kuzingatia maadili katika Utekelezaji wa majukumu yao hasa katika ujazaji wa Matamko yao kwa uadilifu, uwazi na ukweli hasa katika kipindi hiki ambacho viongozi tunajaza matamko yetu kwa njia ya Mtandao.
Mhe, Shigella ametoa kauli hiyo alipokuwa akifungua mafunzo ya Maadili kwa viongozi wa Mkoa wa Geita yaliyoandaliwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Ziwa, yaliyofanyika katika ukumbi wa mkutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita Machi 6, 2025.
Katika hotuba yake Mhe, Shigella amefafanua kuwa kuanzishwa kwa mfumo huu mpya wa ujazaji wa matamko kwa nja ya mtandao umesaidia sana katika kuwarahisishia viongozi kujaza matamko yao kwa haraka kwa usahihi na kwa muda unaotakiwa tofauti na ilipokuwa hapo awali ambapo ujazaji ulikuwa wa kujaza kwenye nakala ngumu.
Ameongeza kuwa uwepo huu wa teknolojia katika ujazaji wa matamko umesaidia pia kuwawezesha viongozi kujaza matamko yao popote pale walipo bila kutumia muda mrefu kusafiri kutoka mkoa mmoja kwenda mkoa mwingine kwa ajili ya kupeleka matamko yao.
Awali akiwakaribisha viongozi Katibu msaidizi Kanda ya Ziwa Bw. Godson Kweka amewataka viongozi wa umma mkoani Geita kutekeleza majukumu yao kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi kwa kutanguliza maslahi ya umma mbele na kukemea vitendo vinavyoashiria ukiukwaji wa maadili ya viongozi.
Mafunzo hayo yamewashirikisha viongozi wa umma wa mkoa wa Geita wakiwemo, wakurugenzi wa Halmashauri, wakuu wa Taasisi, wakuu wa Idara na Vitengo, wakuu wa wilaya pamoja na Kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa.