Viongozi waaswa kujali maslahi ya Umma

Viongozi waaswa kujali maslahi ya Umma
Viongozi wote wa Umma nchini wameaswa kujali maslahi ya Umma ambayo ndiyo msingi mkuu wa Serikali yeyote duniani.
Hayo yalisemwa na Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi alipokua akitoa mada katika kikao cha Viongozi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Tabora kilichofanyika tarehe 06 Agosti 2021 mkoani Tabora.
Mhe. Mwangesi alisema kuwa kiongozi yeyote wa Umma ni kioo cha jamii husika hivyo basi hana budi kujali maslahi ya Umma ikiwa ni pamoja na kuwa mzalendo kwa nchi yake, kufanya kazi kwa uaminifu,huruma,umakini,kijizuia na tamaa na kuzingatia viwango vya juu vya maadili pamoja na kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria taratibu na miongozo mbalimbali.
Mhe.Mwangesi aliongeza kuwa Viongozi wote wanapaswa kuwa na mienendo mizuri isiyotia shaka ili waweze kuaminikakatika jamiiinayowazunguka. Ni dhahiri kuwa kiongozi yeyote anapokua muadilifu kwa watu anaowaongoza bila shaka atapata heshima anayostahili katika jamii nan chi kwa ujumla
Mhe. Mwangesi alisisitiza kuwa “kiongozi ambaye ni muadilifu hufanya mambo mazuri hata pale ambapo hajaambiwa afanye ama pale ambapo hakuna anayemuona lakini kwa yule ambaye si muadilifu anaweza kufanya mambo mengi kwa kutumia nguvu na asifanikiwe hivyo nawaasa viongozi kuwa waadilifu jambo ambalo litarahisishautendaji utendekaji wa yale mambo ambayo wanataka yafanyike”.
Katika hatua nyingine Mhe. Mwangesi aliwakumbusha viongozi baadhi ya misingi ya maadili ikiwa ni pamoja nakufanya maamuzi kwa kufuata sharia,kanuni,miongozo kwa manufaa ya umma,kujiepusha na migongano ya maslahi,kutokua na mienendo ambayo itaaibisha utumishi wa Umma, kuzingatia sheria na mipaka ya matumizi ya madaraka na nyinginezo.
Awali akifungua kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Balozi Dkt Batilda Buriani alisema kuwa Viongozi wote wanapaswa kuwa waadilifu na kuepuka mgongano wa maslahi
Mhe. Batilda alisema kuwa amefurahishwa na ziara ya Mhe Kamishna mkoani hapo kwani ni wazi kuwa ujio wake unawakumbusha viongozi kukumbuka na kujitathmini kupitia kiapo cha Ahadi ya Uadilifu walichoapa mara tuu walipoapishwa kuwa Viongozi.
Kikao hicho cha Kamishna wa Maadili na Viongozi wa Umma ni sehemu ya Maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma mwaka 2021 ambapo Mhe. Mwangesi anatembelea wadau wa maadili, kutoa elimu na kusikiliza kero na malalamiko yao kwa lengo la kuboresha huduma zinazotolewa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma