Viongozi Wa Wa Umma Wametakiwa Kufanya Kazi Kwa Uadilifu

Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi amewataka Viongozi wa umma kufanya kazi kwa uadilifu na uaminifu na kutojiingiza katika vitendo vinavyopelekea ukiukwaji wa maadili hasa mgongano wa maslahi katika utekelezaji wa Majukumu yao ya kila siku.
Mhe. Mwangesi ameyasema hayo katika kikao chake na Viongozi wa Mkoa wa Mwanza kilichokuwa sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma iliyoanza Juni 16 hadi Juni 23, 2022. Kikao hicho kilifanyika katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Kamishna Mwangesi alisema, “jiepusheni na shughuli zinazosababisha mgongano wa maslahi kwasababu mgongano wa maslahi umekuwa chanzo kikubwa cha uvunjifu wa maadili miongoni mwa Viongozi wa Umma.”
Kwa mujibu wa Mhe. Mwangesi, kiongozi wa umma kijihusisha na mgongano wa maslahi ni ukiukwaji wa misingi ya maadili kwani husababisha manung’uniko, kuathiri utendaji na tija kinyume na matarajio jambo ambalo huathiri taswira nzuri ya Serikali mbele ya wananchi.
“Endapo viongozi mtawajibika katika maeneo yanu ya kazi kwa uadilifu itajenga imani kwa wananchi mnaowaongoza na Serikali kwa ujumla,” alisema.
Kamishna Mwangesi aliwataka Viongozi wa mkoa wa Mwanza na Tanzania kwa ujumla kutojiingiza katika Mgongano wa Maslahi wanapotekeleza majukumu yao kwasababu kitendo hicho ni kinyume cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na 13 ya mwaka 1995 kwa mujibu wa ibara ya 132 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
“Ibara hii imekasimu majukumu ya Mhe. Rais yanayotajwa katika kifungu cha 5 (1) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, kusimamia na kukuza uadilifu wa viongozi wa umma,” alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert GabrieL alisema kuwa Maadili ni hatua muhimu inayomtambulisha mtu ndani ya jamii husika na hujitokeza katika matendo yake.
“Maadili tunayozungumza hapa ni maboresho ya maadili yaliyo kwenye vitabu vyetu vya dini na bahati nzuri hapa hakuna mpagani,” alisema na kuongeza kuwa wapo baadhi ya viongozi wanakiuka maadili kwa kula zaidi ya kiasi wanachostahili kula.
“Tule kiasi chetu tulichopangiwa kwa kuwa ukila zaidi ya kiasi chako kitakuletea matatizo na utaishia mikononi mwa vyombo vya dola na kupata fedheha.”
Kwa mujibu wa Mhandisi Gabriel, lengo la kikao hiki ni kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kupinga vitendo vya rusha, ufisadi, na matumizi mabaya ya fedha za Umma.