JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA

OFISI YA RAIS – SEKRETARIETI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA

Viongozi wa Umma watakiwa kutimiza Ahadi ya Uadilifu
27 Oct, 2023
Viongozi wa Umma watakiwa kutimiza Ahadi ya Uadilifu

Viongozi na watumishi wa umma wanaosimamia utoaji huduma katika sekta ya Umma na sekta binafsi watakiwa kuwajibika na kusimamia utoaji wa huduma kwa uadilifu, bila kudai au kupokea rushwa kama walivyokiri katika Ahadi ya Uadilifu.

Hayo yalisemwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Juma alipokua akitoa hotuba yake katika kilele cha maadhimisho ya siku ya maadili na haki za binadamu yaliyofanyika tarehe 10 Desemba, 2022 katika Viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma. Kauli mbiu katika maadhimisho hayo ilikua Maadili,Haki za Binadamu , Utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa ni jukumu la pamoja kati ya serikali, wanannchi na wadau wengine.

Mhe. Jaji Mkuu alieleza kuwa Viongozi na watumishi wa umma wanatakiwa kuwahudumia wananchi kwa weledi, kwa wakati, na kwa viwango vinavyokubalika kama walivyokiri katika viapo vyao vinginevyo wananchi wanayo mamlaka kutwaa dhamana waliyopewa viongozi hao kwa mujibu wa ibara ya 8 ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, Mhe. Jaji Mkuu alieleza kuwa kumekuwepo na vitendo vinavyoashiria ukiukwaji wa ahadi ya uadilifu kwa upande wa viongozi na watumishi wa sekta binafsi jambo ambalo limekua likidumaza maendeleo ya nchi yetu.”Ni lazima Viongozi na watumishi wa Umma tuwajibike, hatuna mbadala na tukubali kuwa wasiowajibika na wasiotoa huduma bora na stahiki kwa wananchi wawajibishwe ” alisema.

Mhe Jaji Mkuu katika hotuba yake aliongeza kuwa kila kiongozi wa umma anapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya Maadili ya Viongozi wa umma ambayo ipo kwa mujibu wa Ibara ya 132 (5)(c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ni pamoja na kupiga marufuku mienendo na tabia zinazopelekea kiongozi kuonekana hana uaminifu, anapendelea au si muadilifu au inaelekea kukuza au kuchochea rushwa katika shughuli za umma au inahatarisha maslahi au ustawi wa jamii.

Mhe Jaji Mkuu alisisitiza kuwa ukosefu wa maadili na vitendo vya rushwavinasababisha wananchi kukosa haki zao “ Tukumbuke kuwa watumishi wa Umma wanaojihusisha na vitendo vya rushwa ni ukosefu wa maadili na wanawakosesha wananchi haki zao za msingi, ustawi wao na wa Taifa kwa ujumla na kwa kufanya hivyo watambue kuwa, wanafanya vitendo vya kijinai na pia wanakiuka Haki za Binadamu na kwamba wanavunja Ibara ya 12-21 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977” alisema.

Pamoja na mambo mengine Mhe. Jaji Mkuu alieleza kuwa Viongozi na watumishi wa umma hawana budi kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwani amekuwa akisisitiza kuhusu uadilifu wa watumishi wanapowahudumia wananchi.Mhe. Rais amekuwa akisisitiza staha na weledi vitumike katika kutimiza majukumu yao ya kila siku ili kufikia malengo ya kuinua uchumi wa chi kwa maslahi ya watanzania wote.

Awali akitoa maelezo ya utangulizi Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Sivangilwa Mwangesi alieleza kuwa tangu mwaka 2016 serikali iliamua kuadhimisha sherehe za siku ya Maadili na Haki za Binadamu ambayo ni muunganiko wa siku mbili ambazo ni Siku ya Kimataifa ya kupambana na rushwa pamoja na siku ya kimataia ya haki za binadamu ambayo huadhimishwa kila tarehe 10 Desemba ya kila mwaka.

Mhe. Mwangesi alieleza kuwa katika kuadhimisha siku ya maadili na haki za binadamu kwa mwaka huu shughuli mbalimbali zilifanyika kuanzia tarehe 06 Desemba 2022 ambazo ni pamoja na Urushwaji wa vipindi maalum vya runinga na redio vilivyotumika kuelimisha umma kuhusu maadili, haki za binadamu utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa. Shughuli nyingine ilikuwa kutembelea magereza ya Isanga kwa lengo la kuongea na kuwasikiliza wafungwa katika magereza hayo na kutoa elimu na huduma kwa Umma katika Viwanja vya Nyerere Square ambapo jumla ya taasisi 16 zilishiriki katika sikuza kutoa huduma kwa Umma.

Aidha Mhe. Kamishna aliendelea kusema kuwa ili kuhakikisha kauli mbiu ya maadhimisho hayo yanawafikia watanzania wengi shughuli mbalimbali zilifanyika katika kanda saba (7) ikiwa ni pamoja na kushiriki katika shughuli katika za kijamii kama vile kutembelea vituo vya kulelea wazee na kutoa misaada, kufanya usafi katika hospitali za mikoa, kutoa elimu ya maadili kwa watumishi waliotembelewa pamoja na kufungua klabu za maadili katika mashule na vyuo mbalimbali.

Maadhimisho hayo ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu huratibiwa na Taasisi zinazosimamia masuala ya Maadili, Mapambano dhidi ya rushwa, uwajibikaji, Haki za Binadamu pamoja na Utawala Bora ambazo ni: Ofisi ya Rais Ikulu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Wizara ya Katiba na Sheria,Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma,Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora,Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa,Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi,Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma pamoja na Tume ya Utumishi wa Umma.

Online Help
Kuanzisha Enzi Mpya katika Udhibiti wa Sekta ya Michezo ya Kubahatisha nchini Tanzania
Ofisi ya maadili inafanya kazi na imewashughulikia viongozi wengi sana kupitia Baraza la Maadili ambalo pia liliendeshwa mwaka 2013 Novemba mkoani Tabora. Viongozi mbalimbali waliokuwa na tuhuma za ukiukaji wa maadili waliitwa kwenye Baraza na kuhojiwa na Baraza linatoa mapendekezo na kuyawasilisha mapendekezo hayo kwa Rais kwa ajili ya hatua zaidi za kinidhamu na kisheria kwa viongozi husika.

" >
Kifungu cha 11(1) cha Sheria ya Maadili kimeainisha wazi mali zinazotakiwa kutajwa kuwa ni fedha taslimu, fedha zilizopo katika taasisi za kifedha kama vile benki, hisa, nyumba, mashamba, magari, mitambo na mali nyinginezo. Kiongozi anatakiwa kutoa tamko la mali anazomiliki yeye mwenyewe, mke/mume na watoto walio chini ya umri wa miaka kumi na nane. Fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni zinatakiwa kujazwa kila mwaka na kiongozi hutumiwa fomu hizo na Ofisi ya Maadili na pia zinapatikana katika mtandao wa maadili yaani www.ethicssecretariat.go.tz. Sheria inamtaka kiongozi kutolea tamko madeni yake ili kuweza kujua kuwa kiongozi anamiliki mali zipi na pia kutambua kuwa amezipata vipi mali hizo ukilinganisha na kipato cha kiongozi husika. Kiongozi kuwa na mali nyingi si dhambi kwani hata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetamka wazi kuwa kila raia ana haki ya kumiliki mali ila ofisi inataka kujiridhisha uhalali wa jinsi mali ilivyopatikana. Mapendekezo katika Katiba mpya yanasisitiza maadili kwa kutenganisha uongozi na biashara.

" >
Wananchi wengi wamejijengea dhana kuwa bila pesa huwezi kupata huduma ya kiserikali kitu ambacho si kweli kwani huduma nyingi za kiserikali zinatolewa bure kabisa ila cha msingi wananchi wanatakiwa kutoa taarifa katika vyombo husika pindi wanapotakiwa kulipia huduma ambazo zinatolewa bure. Jamii inatakiwa kubadilika na kuamini kuwa si lazima kutoa rushwa ndipo upate huduma. Wapo wananchi wengi ambao walileta malalamiko kama hayo na Ofisi ya Maadili iliyashughulikia, hivyo wananchi wasisite kutembelea Ofisi zetu kwa ajili ya kutoa taarifa kama hizo.

" >
Kutoa lugha chafu ni ukiukwaji wa maadili. Ndani ya Bunge kuna Kamati ya Maadili ambayo ipo kwa ajili ya kuwawajibisha wabunge wanaotoa lugha chafu. Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa upande wake ilifanya semina kwa wabunge ili kuwakumbusha mipaka ya utendaji kazi na maadili kwa ujumla, na tangu wakati huo matumizi ya lugha chafu bungeni yamepungua kwa kiasi kikubwa.

" >