VIONGOZI WA UMMA WATAKIWA KUJIEPUSHA NA MGONGANO WA MASLAHI

Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mkoani Kagera Dkt. Abel Nyamahanga amewataka Viongozi wa Umma kuviishi viapo walivyo apa kikiwemo kiapo cha Ahadi ya Uadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao na kuepukana na vitendo vya mgongano wa maslahi ili kujenga imani ya wananchi wanaowaongoza.
Dkt. Nyamahanga ametoa kauli hiyo alipokuwa akifungua mafunzo ya Viongozi wa Umma kuhusu Maadili yaliyoendeshwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba tarehe 23 Januari, 2024.
“Serikali inatumia fedha nyingi kwenye miradi ya maendeleo kupitia katika halmashauri mbalimbali nchini hivyo, rasilimali hizo zinahitaji usimamizi mzuri wa Viongozi” amesema.
Dkt. Nyamahanga ameongeza kuwa Viongozi wa Umma wanayo dhamana kubwa katika kusimamia rasilimali za umma kwa umakini na uadilifu mkubwa ili kujenga imani kwa wananchi wanaowaongoza.
Amewataka viongozi kuzingatia maelekezo ya Serikali katika utendaji wa kazi kwa kufanya maamuzi sahihi kwa lengo la kuwaletea wananchi maendeleo.
Awali akieleza lengo la mafunzo hayo Katibu Msaidizi Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Bw. Godson Kweka aliwakumbusha Viongozi kujiepusha na vitendo vyote vinavyopelekea uwepo wa mgogoro wa maslahi na kuwataka Viongozi hao kufanya kazi kwa uadilifu na uaminifu mkubwa ili kujenga imani kwa wananchi wanaowaongoza.
Bw. Kweka pia amewataka viongozi kusimamia rasilimali za umma kwa uadilifu mkubwa hasa pesa za miradi mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri.
Kuhusu urejeshaji wa Tamko la Rasilimali na Madeni ya Viongozi wa Umma kwa mwaka jana 2023 amesema asilimia 90 ya Viongozi wote wa Halmashauri ya Muleba walirejesh Matamko yao kwa wakati.
Aidha mafunzo hayo ya Maadili ya Viongozi wa Umma yamehudhuriwa na Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba zaidi ya 100 kutoka katika Idara, Vitengo pamoja na waheshimiwa madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo.