Viongozi wa Umma wametakiwa kujiepusha na Mgongano wa Maslahi
Viongozi wa Umma wametakiwa kujiepusha na Mgongano wa Maslahi katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku ili kujenga Imani kwa wananchi wanaowaongoza na Serikali kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mhe. Mwanahamisi Munkunda, alipokuwa akifungua mafunzo ya Maadili kwa Viongozi wa Mkoa wa Mtwara yaliyofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Kanda ya Kusini – Mtwara, tarehe 26 Oktoba 2023.
Mkuu huyo wa Wilaya katika hotuba yake aliongeza kuwa, kiongozi wa Umma anatakiwa kutenda haki kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Umma kwa wananchi anaowaongoza ili kuondoa kero mbali mbali katika maeneo yao ili kujenga Imani ya wananchi kwa Serikali yao.
Mhe. Munkunda alisisitiza kuwa, Viongozi wana wajibu wa kuzingatia Maadili katika kutimiza wajibu wao ili kukidhi mahitaji ya wanannchi mnawaongoza kwa kuhakikisha kuwa misingi, kanuni na taratibu za Serikali zinafuatwa bila ubaguzi na upendeleo wa aina yoyote.
Mhe, Munkunda alibainisha kuwa kiongozi Muadilifu na muwajibikaji anatakiwa kutumia Mali za Umma kwa umakini mkubwa na pia kwa maslahi mapana ya Taifa na wala si vinginevyo.
Aidha, katika hotuba yake pia amefafanua kuwa, Kiongozi wa Umma anatakiwa kutumia cheo chake kwa kutekeleza majukumu yake ya kila siku kwa weledi na uaminifu wa hali ya juu ili kuleta tija kwa wananchi anawaongoza.
Awali akimkaribisha Mgeni Rasmi, Katibu - Idara ya Ukuzaji Maadili, Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Bw. Waziri Kipacha aliwaasa washiriki wa mafunzo hayo kuzingatia yote watakayofundishwa ili kuleta ufanisi katika utendaji wao wa kila siku katika maeneo yao ya kazi.
Mafunzo hayo yamewashirikisha Viongozi kutoka katika Idara, Taasisi na Mashirika mbali mbali ya Mkoa wa Mtwara.