VIONGOZI WA UMMA WAKUMBUSHWA KUREJESHA MATAMKO YAO KWA WAKATI:

Jumla ya Viongozi wa Umma 2,475 kati ya 15,762 ndio wamerejesha Matamko yao ya Raslimali na Madeni hadi kufikia tarehe 20 Desemba 2023.
Taarifa iliyotolewa na Bw. Waziri Kipacha, Katibu Idara ya Usimamizi Maadili Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma tarehe 21.12.2023 jijini Dodoma, imeeleza kuwa idadi hiyo ni sawa na asilimia 16 ya viongozi wote wanaopaswa kurejesha Tamko la Raslimali na Madeni kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995.
Bwana Kipacha katika taarifa yake kwa waandishi wa habari amewataja baadhi ya Viongozi ambao tayari wamekwisharejesha matamko yao kwa kamishna wa Maadili kuwa ni Mhesimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Phillip Mpango, Makamu wa Rais, na Mhe, Kassim Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, Bwana Kipacha amewataka viongozi wengine wa Umma ambao bado hawajawasilisha matamko yao wakiwemo waliotamkwa katika Tangazo la Serikali Na. 857 la tarehe 24 Novemba, 2023 kuwa, “tangu siku ya tangazo hilo wanawajibika kutimiza masharti yote ya Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ikiwemo kuwasilisha Matamko yao kwa Kamishna wa Maadili.”
Katika taarifa hiyo, Katibu huyo amesema kuwa, “kutokana na Mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imeanza kupokea Matamko hayo kwa njia ya Mtandao yaani ‘Online Declaration System- ODS’ ambapo Kiongozi anaweza kuingia katika mfumo kwa anuani ya https://ods.maadili.go.tz au kupitia tovuti ya www.maadili.go.tz na kubofya neno ODS hapo ataingia moja kwa moja na kujaza Tamko lake kwa urahisi zaidi.”
Kwa mujibu wa Bw. Kipacha, mfumo huu utawawezesha viongozi kujaza matamko yao kwa urahisi na kwa usahihi zaidi popote pale watakapokuwa iwe ndani au nje ya nchi na pia utamsaidia kiongozi kutosafiri umbali mrefu na kumpunguzia gharama za kupakua fomu za Tamko kuzijaza na kuzituma kwa njia ya posta ambapo hutumia gharama kubwa na muda mrefu kufika katika ofisi zetu kwa wakati.
Ameitaja faida nyingine ya mfumo wa ODS kuwa ni kuepusha upotevu wa fomu katika zoezi la urejeshaji unaotokana na usafirishaji kwa njia ya posta na vyombo vingine vya usafiri pia mfumo huu utaondoa uwezekano wa kupokea matamko ya watumishi ambao sio Viongozi kwa Mujibu wa Shera ya Maadili ya Viongozi wa Umma na kwamba Kiongozi atakayejaza Tamko atakuwa ametengenezewa akaunti na Sekretarieti ya Maadili.
“Matamko yatakayopokelewa yatakuwa ya Viongozi wanaowajibika na Sheria ya Maadili na Si vinginevyo.” amesema.
Bwana Kipacha amefafanua kuwa, kwa kuzingatia Sheria ya Maadili ya Viongoziwa Umma kifungu cha 9(1)(b) kinamtaka Kiongozi wa Umma kila mwisho wa mwaka kabla ya tarehe 31 Desemba kuwasilisha Tamko lake kwa Kamishna wa Maadili linaloonyesha Raslimali zake, au mume au watoto wake wenye umri usiozidi miaka 18 ambao hawajaoa au kuolewa.