Viongozi wa Umma waaswa kuzingatia Sheria ya Maadili
Viongozi wa Umma wameaswa kuzingatia Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma sura ya 398 wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
Wito huo umetolewa na Katibu Msaidizi Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma Kanda ya Mashariki-Morogoro Bw. Hendry Sawe alipofungua mafunzo ya maadili kwa Viongozi mbalimbali wa Umma na wataalam wa masuala ya TEHAMA kutoka jijini Tanga .
Mafunzo hayo ya siku moja yalifanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Bandari ya Tanga tarehe 05 Machi, 2026.
Bw. Sawe alieleza kuwa Kiongozi yeyote anapaswa kuishi kwa kutii Sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyowekwa na Serikali kwa kuyaishi yale anayoapaa na kuahidi pindi anapoteuliwa ama kuchaguliwa katika nafasi za uongozi.
“Ili Kiongozi aweze kusimamia wenzake ama kukemea maovu lazima awe mfano wa kuigwa na kuishi katika utamaduni wa uadilifu na kuyafanyia kazi kwa vitendo yale aliyoapa wakati alipoteuliwa katika nafasi husika.” alisema.
Bw. Sawe alifafanua kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 6 cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma (sura ya398 marejeo rekebu ya 2023) kimeainisha misingi ya maadili ambayo msingi mojawapo ni kutoa Tamko la Tasilimali na Madeni kwa viongozi wa Umma .
“Kwa muktadha huo ni kuwa suala la Kiongozi kutamka mali zake lipo kisheria hivyo ni wajibu kwa Kiongozi yeyote wa Umma kutii na kuzingatia matakwa haya ili kukuza Imani ya wananchi kwa serikali yao,” alisisitiza.
Katika hatua nyingine Bw. Sawe ameeleza kuwa katika kuhakikisha kuwa Viongozi wanatekeleza takwa hilo bila changamoto Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ilianzisha mfumo wa ujazaji wa Tamko la Rasilimali, Maslahi na Madeni kwa njia ya mtandao ili iwe rahisi kwa Kiongozi kufanya hivyo akiwa popote pale Ulimwenguni.
“Mtakumbuka kuwa tokea kuanzishwa kwa Taasisi hii Viongozi wamekua wakitoa matamko yao kwa njia ya makaratasi lakini sasa tumeamua kwenda kidigitali kama ambayo matamko hayo sasa yanajazwa kwa nja ya mtandao,” alisema.
Pamoja na hayo Bw. Sawe alifafanua kuwa mfumo hu una faida nyingi kwa Viongozi kwani kiongozi anaweza kujaza taarifa zake mahali popote alipo na kwa Taasisi unapunguza muda wa kufanya kazi na kuongeza ufanisi zaidi.
“Mfumo wetu umeunganishwa na mifumo mbalimbali mfano TRA, EGA DAWASA, TANESCO, NIDA, BREALA na mingine mingi kwahiyo ni rahisi kupata taarifa za Viongozi kwa usahihi mkubwa na kuongeza ufanisi wa zoezi hili,” alisema.
Bw. Sawe aliendelea kusema kuwa Sekretarieti imekua ikitoa mafunzo kwa Viongozi lakini imeona ni vyema kutoa mafunzo hayo kwa maafisa TEHAMA ili waweze kuwasaidia Viongozi wengine katika sehemu zao za kazi.
“Tumeamua kutoa mafunzo haya kwa wataalam wa TEHAMA kwa sababu wao wanakaa karibu na baadhi ya Viongozi mfano Wabunge,Madiwani Wakuu wa Idara nk hivyo tuna Imani watatusaidia kuwapatia elimu hii wale walengwa wetu ambao ni Viongozi na kuwapa msaada pale inapobidi”alisema.
Naye mshiriki wa Mafunzo hayo Bi. Aqwilina Kirita Mkuu wa Hazina ndogo jijini Tanga alisema kuwa wamenufaika na mfumo huo kwani umewapunguzia gharama na muda wa kutekeleza zoezi hilo.
“Hapo nyuma tulikua tunasafiri hadi Ofisi za Kanda kuwasilisha Tamko la Rasilimali na Madeni jambo lililokua linatuchukulia muda na pia kutuongezea gharama za usafiri lakini sasa tunajaza kwa urahisi tukiwa mahali popote,” alisema.
Mada mbili ziliwasilishwa katika mafunzo hayo ikiwa ni mada kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma pamoja na mada kuhusu Ujazaji wa Tamko la Rasilimali na Madeni kwa njia ya Mtandao.
.
